Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amesema kutokana na kupungua kwa idadi ya Punda nchini Serikali imesitisha shughuli zote za biashara ya uchinjaji wa mnyama huyo.
Ndaki ameyasema hayo wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2022/2023 hii leo Mei 25, 2022.
Amesema idadi ya punda inazidi kupungua nchini hali inayotishia kutoweka kwa kizazi cha mnyama huyo ambapo idadi ya punda ilikuwa ni 650,000 katika mwaka wa fedha wa 2021/2022.
“Niwataarifu wawekezaji katika machinjio za punda nchini watumie miundombinu ya machinjio hizo kwa ajili ya kuchinja na kuchakata aina nyingine za mifugo kama ng’ombe, mbuzi na kondoo na si punda,”amesema Waziri huyo.
Katika hatua nyingine Waziri huyo wa Mifugo na Uvuvi amesema matukio ya ukamataji na utaifishaji wa mifugo usiofuata utaratibu hasa kwenye maeneo ya hifadhi yamepungua kwa tofauti ya mifugo 6,242,013.
“Matukio ya utaifishaji wa mifugo usiofuata utaratibu maeneo ya hifadhi yamepungua kutoka mifugo 6,245,356 iliyokamatwa mwaka 2020/2021 hadi mifugo 3,343 iliyokamatwa mwaka 2021/2022,’ amefafanua Waziri.
Kupitia hotuba yake hii leo Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeliomba Bunge kupitisha bajeti ya Shilingi 286 bilioni kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ya wizara hiyo.