Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar ametoa maoni yake juu ya namna nzuri kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kila makamu kazi zake zifahamike bila kujali itikadi ya chama chake.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Dar 24 ofisini kwake Zanzibar, Masoud amesema Serikali ya Umoja wa kitaifa haijaanza siku za karibuni ila ni kabla ya Mapinduzi sababu kila kiongozi alitaka kuwa mtawala.
Amesema majukumu ya Makamu wa Pili wa Rais yanaonekana ni mengi kuliko makamu wa kwanza kwa sababu anatoka chama kimoja na Rais hivyo ni rahisi kutekeleza kwa Kuwa yapo kwenye ilani ya chama kinachoongoza Serikali.
“Inawezekana imejengeka dhana kuwa Mimi ama makamu yoyote wa kwanza hana majukumu ya kufahamika ila ieleweke, yule Makamu wa pili ametoka chama kimoja na Rais, inakuwa rahisi kwake kwa kuwa anaenda na ilani ya chama chake kinachoongoza,” amesema.
“Hata Rais lazima awe nae karibu kwa sababu lugha yao ni moja,” ameongeza Masoud.
Mheshimiwa Othman amesema kuna ugumu kuwepo katika serikali ambayo inaongozwa na Kiongozi wa Chama tofauti kwa sababu nyakati nyingi mitazamo haifanani.
“Sisi hatuangalii zaidi ajenda ya Chama chetu, ila tunaangalia zaidi utaratibu wa mfumo wa mambo ambayo tulipaswa kuyafanya kwa maslahi ya wananchi. Nia ni kwamba tumetoka kwenye msukosuko mkubwa hivyo tukae pamoja na kujenga nchi,” amesema Masoud
“Haiwezekani ilani yetu ikaonekana haina jambo hata moja zuri na wala haiwezekani ilani ya CCM sisi tukaiona haina jambo hata moja zuri, hiyo haiwezekani kwa sababu wote tuna ilani ambazo zinataja maendeleo ya nchi na nia yetu kuu ni maendeleo ya nchi,” ameongeza.
Aidha Mheshimiwa Othman amesema kuwa Serikali ya Umoja wa kitaifa ambayo ina maslahi ya chama kimoja inasababisha majukumu husika ya Makamu wa kwanza wa rais kutoeleweka kiutendaji kwa Kuwa yanabaki kwenye katiba na kiuhalisia.
“Kwenye katiba kuna fursa na ilitakiwa mjenge zaidi msiishie pale, hata ukiangalia kazi za makamo wa Rais hazijajieleza vyema wala ufafanuzi wa kutosha, ukitizama kuna mawaziri wanaotoka kwa mujibu wa viti vilivyopatikana, kwa ufupi inaishia hapo, sasa hiyo hamuwezi kujenga mfumo wa Umoja wa Kitaifa kwa kuishia hapo,” amesema mheshimiwa Othman.
Wazanzibari walipiga kura ya maoni Julai 2010 kuidhinisha makubaliano ya kugawana madaraka ya serikali kulingana na matokeo ya uchaguzi mkuu na Matokeo ya kura ya maoni yalionyesha utayari wa Wazanzibari kuweka nyuma uadui na chuki uliotawala kwa muda mrefu.
Angalia mahojiano hayo maalum na Dar 24.