Wito umetolewa kwa wamiliki wa nyumba za wageni na makazi kuandika takwimu za watu wote watakaolala katika makazi yao usiku wa Agosti 23, 2022.
Kamisaa wa sensa ya watu na makazi kwa upande wa Tanzania Bara Anna Makinda amesema hayo katika mkutano maalum na wamiliki wa vyombo vya habari nchini uliofanyika leo mei 27 jijini Dar es Salaam.
Takwimu za sensa zitakazochukuliwa za siku ya Agosti 23 pekee na kuwata wamiliki wa nyumba za malazi na makazi kuhakikisha wanatunza kumbukumbu za watu wote waliolala katika maeneo yao katika usiku huo.
“Makarani wa sensa wanaweza kuchelewa kuyafikia makazi yako kwa ajili ya zoezi la kuhesabiwa, wanaweza kuja hata tarehe 25 au 26 huko, lakini watahitaji takwimu za watu waliolala hapo siku ya tarehe 23, hivyo ni muhimu kuandika pembeni ili usisahau na kusaidia kutoa taarifa sahihi itakayowezesha kupata takwimu sahihi na bora zaidi,” amesema Makinda.
Makinda amesema kuwa zoezi la sensa ya watu na makazi mwaka huu litafanyika kwa mfumo wa kidigitali ambapo takwimu zitakazokusanywa zitajazwa moja kwa moja kwenye kishikwambi (tablet) na kutumia mifumo ya tehama kuhesabu na kuhifadhi takwimu hizo
Zoezi hilo pia linatarajiwa kwenda sanjari na uhakiki wa anuani za makazi na majengo hivyo makarani wa sensa watapatiwa mafunzo maalumu kwa muda wa siku 21 ili kupata uelewa wa kutosha kuhusu mifumo hiyo inayoambatana na sensa ya watu na makazi kwa mwaka huu.
Hii ni sensa ya sita kufanyika tangu kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo sensa ya kwanza ilifanyika mwaka 1967 chini ya uongozi wa Rais Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Mara ya mwisho zoezi la sensa ya watu na makazi lilifanyika mwaka 2012 ambapo jumla ya watu milioni 44.9 walihesabiwa.
Jumla ya watu milioni 61 wanatarajiwa kuhesabiwa katika sensa ya mwaka huu.