Mshambuliaji kutoka Uruguay Edinson Roberto Cavani Gómez amewataja Cristiano Ronaldo na David De Gea kama wachezaji bora kwenye kikosi cha Manchester United kwa msimu wa 2021/2022, uliofikia tamati majuma mawili yaliyopita.

Manchester United ilimaliza msimu ikiwa nafasi ya 6 katika msimamo wa ligi ya England, licha ya kupewa nafasi kubwa ya kufanya vyema kutokana na kuwa na wachezaji wenye uzoefu katika Mshike Mshike wa Soka Barani Ulaya.

Cavani ambaye hatokuwa sehemu ya kikosi cha Manchester United msimu ujao, amesema Ronaldo na De Gea walikua tofauti na wachezaji wengine klabuni hapo, kutokana na kuonyesha uhodari na uimara wakati wote wa msimu.

Amesema wawili hao walisababisha mambo mengi ya kuikoa Manchester United pale ilipokua katika hali ngumu kwenye michezo ya Ligi Kuu ya England, huku akimini huenda mawazo yake binafsi yakuwakubali wachezaji hao yakaungwa mkono na Mashabiki wa klabu hiyo.

“Nadhani mchezaji bora kwetu msimu huu na mtu ambaye alionyesha uthabiti zaidi, akicheza vizuri mara kwa mara na kila wakati yupo kwa ajili yetu, Cristiano mbali na kuwa na kipindi kifupi ambapo hakuwa akifunga bao, ambapo inaweza kutokea ukiwa mshambuliaji, Cristiano labda alikuwa mchezaji wetu mmoja ambaye alionyesha uimara zaidi “

“Kwa De Gea pia amekuwa mmoja wa wachezaji waliocheza vizuri zaidi kikosini, kwa hivyo kwa pamoja, wamekuwa wachezaji imara na bora zaidi kikosini katika msimu wetu wakati huu” amesema Cavani

Cavani akiwa Manchester United tangu mwaka mwaka 2020 hadi mkataba wake ulipomalizika mwaka huu 2022, ameitumikia klabu hiyo katika michezo 41 na kufunga mabao 12.

Alisajiliwa klabuni hapo kama mchezaji huru, baada ya kuachana na mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain, ambako alicheza michezo 200 na kufunga mabao 138, akicheza tangu mwaka 2013 hadi 2020.

Watalii zaidi ya 50 kupanda Mlima Kilimanjaro kwa baiskeli
Gwajima:Wanawake kaeni mstari wa mbele kukomesha ukatili