Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekemea tabia ya utiririshaji wa maji machafu na majitaka kutoka viwandani na kwenye migodi kwani inahatarisha usalama wa afya ya binadamu na mazingira.
Majaliwa ametoa onyo hilo leo Jumapili, Juni 5, 2022 wakati akizungumza na wadau mbalimbali walioshiriki kilele cha maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo kitaifa yamefanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.
Amesema, “hivi karibuni tumeshuhudia kutoweka kwa baadhi ya viumbe hai, maeneo mengi ya vyanzo vya maji yameathirika kutokana na ukame wa mara kwa mara, uchafuzi wa mazingira unaotokana na majitaka na kemikali kutoka na shughuli za viwandani,”
Ameongeza, “uchafuzi huu umeendelea kuongezeka kwa kasi nchini na kuathari maji, hewa na ardhi. Hali hii inahatarisha usalama wa afya ya bidamu na mazingira.”
Vilevile, amekemea tabia ya uchomaji miti, uvamizi na uharibifu wa mapori tengefu, ukataji wa miti holela kwa ajili ya uchomaji wa mkaa, uvamizi na uharibifu wa vyanzo vya maji pamoja na uchomaji moto misitu.
“Kutokana na kuongezeka kwa uharibifu wa mazingira, ninaagiza Wizara na taasisi husika, pamoja na wananchi kwa ujumla, kuimarisha ushirikiano katika kukomesha uvamizi na uharibifu wa mapori tengefu kote nchini. Ninawasihi wananchi tutoe ushirikiano wa kutosha kuhakikisha tunarejesha misitu, ikolojia na uoto wa asili katika maeneo yetu, hususan maeneo ambayo miti ya asili iko kwenye tishio la kutoweka. Tuwe walinzi wazuri wa mazingira kwa faida ya kizazi hiki na kijacho,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamiu wa Rais anayeshughulikia mazingira, Dkt. Suleiman Jafo amesema ofisi yake imezindua mpango wa soma na mti ambapo kila mwanafunzi anapaswa kupanda mti mmoja.
“Tumezindua kampeni ya Soma na Mti ambapo wanafunzi milioni 14.5 kutoka shule za msingi, sekondari na vyuo vikuu wameshiriki kwa kupanda mti mmoja mmoja.
Waziri Mkuu alizindua Mpango Kabambe wa Hifadhi ya Mazingira na kutoa tuzo kwa Mabalozi wa Mazingira na viongozi wakuu watano akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.
Kaulimbiu ya siku ya mazingira ni ‘Tanzania ni moja tu, Tunza Mazingira.’