Uongozi wa klabu ya Biashara United Mara inayopambana kujinusuru kushuka daraja msimu huu, umetangaza kuachana na Kocha Mkuu Vivier Bahati sambamba na wasaidizi wake leo Jumatatu (Juni 06). 

Maamuzi hayo yamefikiwa, kutokana na hali ya kutoelewana kati ya Kocha Mkuu na baadhi ya maafisa wengine wa Benchi la Ufundi, hali ambayo inadhaniwa kuwa chanzo cha matokeo mabovu yanayowaandama. 

Kocha Bahati anaondoka Biashara United Mara, baada ya kufanya kazi klabuni hapo kwa miezi mitano tangu alipoajiriwa, akichukua nafasi ya Moses Odhiambo aliyetimka mwishoni mwa mwaka jana 2021. 

Vivier alitambulishwa Januari 18, 2022 kuwa kocha mkuu wa wanajeshi hao wa mpakani baada ya kupewa kandarasi ya miezi sita tu.

Hadi sasa Uongozi wa klabu hiyo haujaainisha jina la Kocha atakayerithi mikoba ya Vivier Bahati, huku Ligi Kuu ikitarajiwa kuendelea tena mwishioni mwa juma hili. 

Biashara United Mara hadi sasa ina michezo minne dhidi ya Kagera Sugar (Ugenini), Geita Gold (Ugenini), KMC FC (Nyumbani) na Azam FC (Ugenini). 

Hadi sasa Biashara United Mara ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa alama 24, baada ya michezo 26. 

Katika kuhakikisha timu hiyo inabaki Ligi Kuu Biashara United Mara imejizatiti kukusanya alama 10 kati ya 12 kwenye michezo yao iiyosalia msimu. 

Young Africans kuanzia hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika
Amuua mama yake akitaka mali