Mamlaka ya kijeshi nchini Mali imeweka muda wa mpito wa uongozi wake unaofikia miezi 24 ukiwa na lengo la kurejesha utawala wa kiraia hapo Machi 2024, kufuatia mapinduzi yaliyotokea mara mbili nchini humo.

Kupitia televisheni ya Serikali, msemaji wa mamlaka ya mpito Abdoulaye Maiga amesema taarifa ambayo ni amri iliyotiwa saini na mtawala wa sasa Assimi Goïta imesema wataongoza kwa kipindi hicho ili kuweka mambo sawa.

“Muda wa mpito umewekwa kuwa miezi 24 hadi Machi 26, 2024, kwa mujibu wa kifungu cha 22 cha sheria cha Februari 25, 2022 kinachorekebisha hati ya mpito”, amesema Abdoulaye.

Hata hivyo, taarifa hii inakuja ikiwa ni siku chache baada ya mkutano wa ECOWAS SUMMIT, ulioweka kizuizi cha kikanda nchi ya Mali tangu Januari 2022 na kukataa kile walichokiita ratiba isiyokubalika kwa uongozi wa nchi hiyo ya kurejesha utawala kwa serikali ya kiraia.

Februali 2022, Bunge la Mali liliidhinisha katiba inayoruhusu mabadiliko ya kidemokrasia ya miaka mitano, huku kamati ya kiufundi ya ECOWAS ikipendekeza kupangwa kwa upigaji wa kura ndani ya miezi 12 au 16.

Choguel Maiga, Waziri Mkuu aliyewekwa madarakani na jeshi la Mali amesema “Hatuwezi kwenda chini ya miezi 24 isipokuwa tuamue kuahirisha au kutofanya hatua fulani hadi mwisho.”

Licha ya mazungumzo kati ya mpatanishi wa ECOWAS na serikali ya Goïta, pande zote mbili zimeshindwa kukubaliana kuhusu muda wa maafikiano na bado kitengo cha kikanda hakijatoa maoni kuhusu kipindi hicho cha mpito kilichotangazwa na watarajia kukutana tena Julai 3, 2022.

Wanahabari wapaza sauti maboresho ya sheria
Laki nne wafa kwa kula chakula kisicho salama