Klabu ya Simba inahusishwa na mpango wa kumsajili Kiungo kutoka nchini Mali na klabu ya Red Arrows ya Zambia Allasane Diarra, ikiwa sehemu ya mkakati wa klabu hiyo wa kuboresha kikosi chake kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa.
Msimu huu 2021/22 Simba SC imepoteza ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’, huku ikishindwa kufikia lengo la kucheza Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Simba SC inatajwa kuwa kwenye mpango wa kumnasa Diarra, kufuatia kuridhishwa na uwezo wake kisoka, na tayari aliwahi kucheza dhidi ya wababe hao wa Msimbazi katika mchezo wa Mchujo wa Kombe la Shirikisho jijini Dar es salaam (Tanzania) na Lusaka (Zambia) mwishoni mwa mwaka 2021.
Usajili wa kiungo huyo unatajwa kuwa sehemu ya mapendekezo yaliyoachwa na Kocha Pablo Franco Martin, ambaye mwanzoni mwa juma lililopita alivunjia mkataba wake, kwa kigezo cha kushindwa kufikia malengo aliyowekewa na Uongozi wa Simba SC.
Pablo alipendekeza usajili wa kiungo kiungo mshambuliaji mmoja wa kigeni, kupitia ripoti yake ambayo aliiwasilisha kwa viongozi, kabla ya kuondoka nchini.
Hata hivyo imeelezwa kuwa jina la Diara limepitishwa na viongozi wa Simba SC, baada ya mchakato wa kupitia majina mengine ya viungo washambuliaji wanne, ambao walipendekezwa kusajiliwa klabuni hapo.
Viongo wengine ambao walijadiliwa na jopo la viongozi wa Simba SC ni Victorien Adebayor anayehusishwa na mpango wa kusajiliwa na Mabingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika RS Berkane ya Morocco, Morlaye Sylla na Stephane Aziz Ki anayehusishwa na Young Africans.
Diarra aliyezaliwa Januari 8, 1997 amewavutia Simba SC kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira, kupiga pasi zenye kuanzisha mashambulizi, kufunga mabao na kuwasumbua viungo wa timu pinzani.
Simba SC imepanga kusajili kiungo mmoja wa ushambuliaji kutokana na kutokuridhishwa na kiwango cha Clatous Chama, Rally Bwalya ambaye dili lake la kutua Amazulu likikamilika anaweza kutimka ikiwemo viwango vya nyota wengine wa nafasi hiyo kutokuwa bora.
Katika hatua nyingine Simba SC watakuwa na nafasi ya kuongeza wachezaji wa kigeni baada ya kuacha na Benard Morrison huku Pascal Wawa, Meddie Kagere na Taddeo Lwanga nao wanatajwa kutemwa mwishoni mwa msimu.