Afisa Mtendaji Mkuu wa Namungo FC, Omar Kaaya amethibitisha taarifa za kuondoka kambini kwa Mshambuliaji wa klabu hiyo David Molinga ‘FALCAO’ ambaye anadaiwa kuzua taharuhi kwa Mashabiki wa klabu hiyo ya mkoani Lindi.

Molinga alisajiliwa Namungo FC mwanzoni mwa msimu huu akitokea ZANACO FC ya Zambia, lakini siku karibuni amekua hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi cha kwanza cha klabu hiyo.

Kaaya amesema ni kweli Mshambuliaji huyo ameondoka Kambini, lakini sio kama inavyoelezwa katika baadhi ya Vyombo vya Habari na Mitandao ya kijamii ambapo inasemeakana ametoroka na kutokomea kusikojulikana.

Kiongozi huyo amesema Molinga ameondoka Namungo FC kwa utaratibu maalum, na kwa sasa yuko nchini kwao DR Congo baada ya kupewa mapumziko, kupisha michezo ya Kimataifa.

“Kila mtu ana uhuru wa kuzungumza analolijua, ila ukweli ni kwamba Molinga na wenzake wamepewa mapumziko kwa ajili ya kupisha kalenda ya michezo ya kimataifa inayoendelea na sio vinginevyo kama inavyosambazwa,” amesema Kaaya.

Samatta awaita watanzania Kwa Mkapa
Kanoute: Diarra akitua Simba SC itakua balaa