Uongozi wa Biashara United Mara umemtangaza Kocha Khalid Adam kuwa Kocha Mkuu wa kikosi cha klabu hiyo, baada ya kuachana na Kocha Vivier Bahati mwanzoni mwa juma hili.

Biashara United Mara umefanya maamuzi hayo kwa haraka ili kuiwezesja timu yao kuwa na maandalizi bora kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar, utakaopigwa mwanzoni mwa juma lijalo.

Tayari Kocha Khlid Adam ameshaanza kazi ya kukinoa kikosi chake mjini Musoma Mkoani Mara, huku akiwataka Mashabiki na Wafanyabiashara mkoani Mara kuungana kwa Pamoja ili kuipa nguvu timu yao.

Amesema jukumu lililo mbele yake ni kubwa, lakini huenda likawa dogo na rahisi endapo Wadau wote wa Soka mkoani Mara watampa ushirikiano wa kutosha, katika harakati za kuinusuru Biashara United Mara iliyo kwenye janga la kushika daraja msimu huu.

“Nimeona timu ina muelekeo wa kuweza kubaki Ligi Kuu kwa msimu ujao, kikubwa ninaomba ushirikiano kutoka kwa kila Mdau wa Soka mkoani mara ili kukamilisha zoezi hili ambalo kwangu ni zito, lakini huenda likawa jepesi kama ushirikiano utakuwepo.”

“Nimeona wachezaji waliopo kikosini ni wazuri, wanaweza kupambana na kupata matokeo katika michezo inayotukabili, hii imenipa moyo wa kukubali kufanya kazi katika klabu hii, kwa sababu ninaona kuna jambo linakwenda kutokea kwa mafanikio.” Amesema kocha Khalid Adam

Kwa mara ya mwisho Kocha Khalid Adam alikiongoza kikosi cha Mwadui FC ya mkoani Shinyanga iliyokua inashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara misimu miwili iliyopita.

Biashara United Mara hadi sasa ina michezo minne dhidi ya Kagera Sugar (Ugenini), Geita Gold (Ugenini), KMC FC (Nyumbani) na Azam FC (Ugenini).

Hadi sasa Biashara United Mara ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa alama 24, baada ya michezo 26.

Wachezaji Biashara United Mara waahidi makubwa
Young Africans yatuma ujumbe Tanga, yatamba kuibanjua Coastal Union