Uongozi wa Biashara United Mara umeendelea kuwahimiza Mashabiki wa Soka na Wafanyabiashara mkoani Mara, kuwa sambamba na timu yao katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu huu 2021/22.

Biashara United Mara inahitaji kushinda michezo minne iliyosalia, ili kujinusuru na janga la kushuka daraja, ambalo linaendelea kuinyemelea kutokana na matokeo ilioyapata siku za karibuni.

Katibu Mkuu wa Biashara United Mara Mariam Derick amesema, Uongozi unaendelea kupambana ili kuhakikisha timu hiyo haishuki daraja, na ndio maana wamejitahidi kumuajiri Kocha Khalid Abeid kwa haraka, ili kuziba nafasi ya Kocha Vivier Bahati aliyeondoka na maafisa wake wa Benchi la Ufundi mwanzoni mwa juma hili.

Amesema Mashabiki wa Soka na Wafanyabiashara mkoani Mara wanatakiwa kuwa bega kwa bega na timu yao, ambayo mwanzoni mwa juma lijalo itakabiliwa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar.

“Tunaendelea kuhimiza mshikamano wa kila mmoja wetu mkoani Mara, tunaamini katika umoja ili kuvuka katika kipindi hiki kigumu, kila mmoja wetu akipambana kwa kuhimiza mshikamano, ninaamini tutafanikiwa.”

“Viongozi tumepambana usiku na mchana na kufanikiwa kumpata Kocha Adam ambaye amekubali kujiunga nasi katika vita ya kuibakisha klabu yetu Ligi Kuu, sasa ni jukumu letu wote kumpa ushirikiano na kuipa nguvu timu yetu ili ifanikiwe.” Amesema Mariam

Biashara United Mara hadi sasa ina michezo minne dhidi ya Kagera Sugar (Ugenini), Geita Gold (Ugenini), KMC FC (Nyumbani) na Azam FC (Ugenini).

Hadi sasa Biashara United Mara ipo nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa alama 24, baada ya michezo 26.

Kagera Sugar yasaka alama 12 Ligi Kuu
Wachezaji Biashara United Mara waahidi makubwa