Baada ya kupoteza mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa ‘KUNDI F’ wa kuwania kufuzu Fainali za AFCON 2023 dhidi ya Algeria, Wachezaji wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania ‘TAIFA STARS’ wamezungumzia matokeo hayo, huku wakiamini bado kuna nafasi ya kufuzu.
‘TAIFA STARS’ ilipoteza mchezo huo kwa mabao 2-0, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam juzi Jumatano (Juni 08), baada ya kulazimisha zare ya 1-1 dhidi ya Niger ugenini, siku ya Jumamosi (Juni 04).
Aliyekua Mshambuliaji wa Simba SC, Mtibwa Sugar, Mlandege ya Zanzibar na Timu ya Taifa Dua Said amesema, hana shaka na kikosi cha Taifa Stars chini ya Kocha Kim Poulsen, kutokana na jitihada alizoziona kwenye michezo yote miwili.
Amesema bado kuna nafasi ya kuendelea kupambana na kutimiza lengo la kufuzu AFCON 2023, kutokana na msimamo wa ‘KUNDI F’ ulivyo hadi sasa, hivyo amewahimiza watanzania kuendelea kuwa na imani na kikosi chao.
“Binafsi nilitazama michezo yote miwili, nimeona wachezaji wetu wana ari ya kujituma, ninaamini wakiendelea na mpango huo kuna kitu wanaweza kukipata na kufuzu AFCON 2023, kupoteza dhidi ya Algeria ni sehemu ya matokeo ya mchezo, japo hatukutarajia hilo kutokea katika Uwanja wa nyumbani,”
“Pamoja na kupoteza mchezo, bado kuna mipango ya timu ilionekana na kuna nafasi ambazo zilitengenezwa, lakini haikua bahati kwetu kupata ushindi dhidi ya Algeria, ninaamini hakuna kinachoshindikana kwa sababu Kocha ameona wapi tulipokosea, tutafanya vizuri katika michezo inayofuata.” amesema Dua Said
Naye Mlinda Lango wa zamani wa Young Africans, Pan Africans na Taifa Stars, Juma Pondamali bado kuna tatizo ambalo ameliona kwenye mkakati wa kuiwezesha Timu ya Taifa kufanikisha lengo la kufuzu AFCON 2023, ukilinganisha na mataifa mengine ambayo yanawania Tiketi ya kucheza Fainali hizo nchini Ivory Coast.
Pondamali amesema Serikali kwa kushirikiana na TFF inapaswa kurejesha Kamati ya ‘Saidia Taifa Stars Ishinde’ ili kuongeza Morari kwa wachezaji ambao wanapambana kwa ajili ya Taifa lao.
“Kuna kitu kimepungua kweye timu yetu, kuna haja ya ile kamati ya ‘Saidia Taifa Stars Ishinde’, hii kamati ina uzito wake wa kuongeza Morari kwa wachezaji wetu, ninaamini kama itakuwepo na ahadi zikatolewa kwa wachezaji nina uhakika kuna makubwa tutayaona kuliko haya tuliyoyaona,”
“Hawa wachezaji ukiaaambia mkimpiga mtu tunakupeni kila mtu Ghorofa, ninakwambia kila mchezaji atapambana ili apate hilo Ghorofa! ama unaweza kuwaambia mkimpiga mtu tutakupeni Mabenz, mimi ninakwambia tutaona juhudu zaidi kwa wachezaji wetu!” amesema Pondamali.
Taifa Stars itaendelea kusaka Tiketi ya kucheza Fainali za AFCON 2023 mwezi Septemba, kwa kuikabili timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ itakayokua nyumbani St. Mary’s Stadium-Kitende, mjini Entebbe. Hadi sasa msimamo wa Kundi F unaonyesha Algeria inaongoza ikiwa na alama 6, ikifuatiwana Niger yenye alama 02, Tanzania na Uganda zinalingana zikiwa na alama moja kila mmoja.