Msichana mmoja mwenye umri wa miaka 10 amekamatwa Juni 7, nchini Marekani baada ya kudaiwa kumpiga risasi mwanamke ambaye alikuwa akizozana na mama yake.

Taarifa za Idara ya Polisi ya Orlando, Marekani mtoto huyo aliwekwa chini ya ulinzi wa Idara ya Watoto na Familia ya Florida kuwa mama wa mtoto huyo pia amezuiliwa.

Katika taarifa yake, Mkuu wa Mashtaka ya Serikali ya Kaunti za Orange na Osceola, Monique H. Worrell alisema ofisi yake imeanza kushughulikia kesi hiyo na itazingatia ukweli wote, ikiwa ni pamoja na umri wa mtoto huyo, na mazingira yake wakati kutoa uamuzi.

Kwa mujibu wa shirika la habari la CNN, Worrell alisema kwamba hakuna uamuzi wowote umetolewa na ofisi yake akiongeza kuwa tukio hilo ni moja ya kesi za kusikitisha ambazo hajawahi kushuhudia katika miaka 22 ya taaluma yake.

Taarifa zinasema kisa hicho kilitokea usiku wa Mei 30, wakati mama wa mtoto huyo na mwathiriwa, Lashun Denise Rodgers, walipoanza kuzozana nje ya jengo la ghorofa.

Mtoto huyo alikuwa na mama yake wakati wa mabishano hayo, na kwa mujibu wa ripoti ya mashahidi na inasemekana Mama huyo anadaiwa kuanzisha ugomvi kwa kumpiga Rodgers, ambaye alilipiza kisasi kwa kumpiga mgongoni kama alivyoeleza rafiki wa marehemu.

Rafiki huyo wa Rodgers alijaribu kuwatenganisha wawili hao lakini mwathiriwa alijaribu kuendelea tena kupigana na mama huyo.

Inadaiwa kuwa alimwona mtoto huyo akiwa ameshika bunduki nyeusi kabla ya kufyatua risasi mbili kwa Rodgers.

Baada ya kutekeleza kitendo hicho, mtoto huyo anadaiwa kupiga kelele akisema Rodgers hakupaswa kumpiga mama yake.

Msemaji wa polisi Heidi Rodriguez alisema kuwa Rodgers alipelekwa Kituo cha Matibabu cha Mkoa cha Orlando ambako alifariki baadaye.

Ajali nyingine Lushoto, watano wafariki
Monkeypox 'yabisha' hodi Uganda