Zaidi ya watu 50 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa, katika matukio mawili tofauti likiwemo la anga lililofanywa na Helkopta isiyofahamika eneo la Serikali ya Mtaa wa Kajuru lililopo Jimbo la Kaduna nchini Nigeria.

Wakisimulia kutokea kwa tukio hilo, baadhi ya Wanakijiji wamesema hawakuweza kuitambua mara moja Helikopta hiyo kutokana na kila mmoja kujaribu kuyaokoa maisha yake na ilitoweka baada ya mkasa huo.

“Tunahisi watakuwa ni magaidi wa umwagaji damu maana lilikuwa ni shambulio la ghafla sijui wanataka nini hawa watu ni juzi tu wameteka watu sasa tena leo wamekuja na jingine,” alilalamika mmoja wa Wanakijiji Frank Echukwu.

Amesema shambulio hilo lililenga Vijiji vya Ugwan Gamu, Dogon Noma, Ungwan Sarki, na Maikori vilivyopo Halmashauri ya Kajuru na kwamba hawakuitilia maanani Helkopta hiyo wakati ikiwasili na kwamba Pikipiki nyingi pia ziliwasili na zikawashambulia.

“Hili tukio linatokea ikiwa ni chini ya saa 24 baada ya magaidi kuwateka nyara watu wengine 14 katika Kituo cha Iri kipo kilomita 8 kutoka mji wa Idon, Halmashauri ya Kajuru,” alisimulia Mama mmoja aliyekuwa na mtoto Mariane Oju.

Inadaiwa Juni 3, 2022, Magaidi hao waliwauwa wenyeji 25 baada ya kupatikana kwa miili mingine saba porini, wakati wanakijiji hao walipokuwa wakipita vichaka vilivyozunguka mji huo kutafuta maiti kufuatia shambulio la awali.

Mama huyo ameongeza kuwa, “Wapiganaji walikuja mara mbili na kufanya operesheni bila kizuizi, walikuja wakihisi kwamba hakutakuwa na tishio kutoka kwa mtu yeyote”.

“Wakati baadhi ya watu wetu walipotekwa nyara nao siku ya Jumamosi lilikuwa ni jambo la kawaida maana tumezoea, lakini tulifikiri hiyo ilikuwa imetosha kumbe wana mipango zaidi hatukuweza kulala usiku huo,” aliongeza Bi. Oju.

Rais wa Kitaifa wa Jumuiya ya eneo hilo, Awemi Dio Maisamari ameongea na vyombo vya Habari na kusema shambulio hilo lilianza majira ya saa sita mchana na lilidumu hadi saa kumi na mbili jioni bila kizuizi.

Amesema shambulio hilo lilitekelezwa na magaidi ambao walipanda pikipiki takriban 150 wakiwa wamebeba watu watatu wenye Bunduki aina ya AK-47 kila mmoja kwa usaidizi wa Helikopta hiyo iliyokuwa angani.

Uhasama DRC, Rwanda washika kasi
Mongella athibitisha kifo cha askari Loliondo