Kiungo Mshambuliaji kutoka DR Congo Deo Kanda, huenda leo Jumatatu (Juni 13), akaonekana kwa mara ya kwanza akiwa na kikosi cha Mtibwa Sugar, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting.
Miamba hiyo itaonyeshana undava katika Uwanja wa Manungu Complex Mkoani Morogoro kuanzia saa nane mchana, huku kila mmoja akihitaji alama tatu muhimu ili kujiondoa kwenye shimo la kushuka daraja.
Taarifa kutoka Mtibwa Sugar zimeeleza kuwa, Kiungo huyo ambaye aliwahi kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara misimu miwili iliyopita akiwa na Simba SC, ana uhakika wa kucheza kwenye mchezo dhidi ya Ruvu Shooting baada ya kupata Kibali cha Uhamisho wa Kimataifa ‘ITC’ kutoka kwenye klabu ya TP Mazembe iliyokua inamimliki kabla ya kusaini Mtibwa Sugar, wakati wa Dirisha Dogo la Usajili.
Kwa zaidi ya miezi mitano, Mtibwa Sugar walipambana kupata Kibali cha Uhamisho wa Kimataifa cha mchezaji huyo kwa usaidizi wa Shirikisho la soka nchini TFF, na hatimaye wamekipata, huku michezo minne ikisalia kabla ya kumalizika kwa msimu huu 2021/22.
Usajili wa Deo Kanda ulichagizwa na hitaji la wachezji wenye uzoefu katika kikosi cha Mtibwa Sugar, kufuatia mambo kuwaendea kombo msimu huu 2021/22, na hii ni mara ya tatu mfululizo kwa klabu hiyo kuingia katika orodha ya timu zilizo katika hatari ya kushuka daraja.
Mtibwa Sugar iliyoshuka Dimbani mara 26 hadi sasa, imejikusanyia alama 28 zinazoiweka kwenye nafasi ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu, huku Mpinzani wake mtarajia Ruvu Shooting akiwa nafasi ya 13 baada ya kucheza michezo 26 na kukusanya alama 28.