Waziri Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba amesema katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali itaendelea kukamilisha miradi ya kielelezo na ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Waziri Nchemba, amesema hayo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Amesema miradi hiyo ya kielelezo na ya kimkakati inatarajiwa kuzalisha ajira, kuongeza kipato pamoja na kupunguza hali ya umaskini nchini.
Dkt. Nchemba ameitaja miradi hiyo kuwa pamoja na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (SGR), mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere, kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) huko mkoani Lindi.
Aidha, ameongeza kuwa miradi ya kipaumbele kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 itaendelea kuzingatia maeneo matano ya kipaumbele ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano kuanzia mwaka 2021/2022 hadi 2025/2026.
Alasiri ya leo juni 14, 2022, Dkt. Nchemba anatarajiwa kuwasilisha bungeni bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.