Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dkt. Wilson Mahera Charles amewataka watanzania kuwa tayari kushiriki kikamilifu zoezi la kuhesabiwa wakati wa sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23, 2022 nchini kote.

 Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dododma, Dkt. Mahera amesema zoezi hilo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi, kwani hata Tume ya Taifa ya Uchaguzi hutegemea takwimu za sensa kukadiria idadi ya wapiga kura wapya.

“Wapiga kura au shughuli za uchaguzi kwa ujumla zina uhusiano mkubwa na takwimu zitokanazo na sensa, katika sensa ndipo Tume inaweza kubainisha idadi ya watu itakayowaandikisha katika daftari la kudumu la mpiga kura,” amesema Dkt. Mahera

Amesema “Nawahimiza watanzania kujitokeza kuhesabiwa kwenye sensa ya watu na makazi mwaka huu na kila mmoja kumhamasisha mwenzake kuhesabiwa.”

Aidha, amesisitiza kuwa ili Tume iweze kufanya shughuli zake vizuri, ni lazima ipate takwimu sahihi za watu, makazi na kutambua makundi maalum ambayo ni ya Wanawake, Wazee, Vijana na watu wenye Ulemavu.

“Sensa ya mwaka huu itafanyika kidijiti na itaweza kubainisha idadi ya majengo ya umma ambayo sisi huyatumia kuweka vituo vya kujiandikisha, lakini pia itatusaidia kuweka vituo kwa mujibu wa anuani za makazi,” amesema Dkt Mahera.

“Tume imekua ikipanga mipango yake kwa takwimu kuanzia ngazi ya kata lakini sasa kwa kuwa sensa inakwenda kuweka kumbukumbu hadi ngazi ya kitongoji, Tume itaweza kupanga mipango yake kwa urahisi zaidi na matumizi ya teknolojia katika uchaguzi yataongezeka,” amefafanua Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi.

Sensa ya watu na makazi hufanyika kila baada ya miaka 10 na mara ya mwisho Sensa hiyo ilifanyika mwaka 2012 ambapo watanzania milioni 44,929 walihesabiwa. 

KMC FC yaanza kuiwinda Simba SC
Adel Zrane: Ninafahamu kinachoendelea Simba SC