Jumla ya watu 20 akiwemo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ngorongoro, Ndirango Laizer wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa shitaka la mauaji ya kukusudia ya askari Polisi Garlus Mwita (36), yaliyotokea Juni 10, 2022.

Waliofikishwa Mahakamani mbali na Laizer ni madiwani wa CCM wa baadhi ya Kata za Loliondo akiwemo Molongo Pachal, Albert Selembo, Simeli Parwat, Lekayoko Parmwati, Sapati Parmwati, Ingoi Kanjwel, na Sangai Morongeti.

Wengine ni Morijoi Parmati na Morongoti Meeki, Shengena Killel, Kambatai Lulu, Moloimeti Yohana, Ndirango Laizer, Kijoolu Kakeya, Simon Orosikiria, Damian Laiza, Mathew Eliakimu, Luka Kursas, Talengo Leshoko na Joel Lessonu.

Watuhumiwa hao walisomewa mashtaka na baadaye kupelekwa gereza Kuu la Kisongo lililopo Jijini Arusha kwa kuwa tuhuma za mauaji zinazowakabili hazina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Juni 17, 2022, Mbunge wa Ngorongoro (CCM), Emmanuel Ole Shangai alitoa taarifa ya kutojulikana walipo viongozi kumi wa Wilaya hiyo, akiwemo Mwenyekiti huyo wa CCM na madiwani hao wanaotajwa kufikishwa Mahakamani.

Garlus aliuawa katika eneo la Loliondo, akiwa na askari wenzake katika kazi ya kuimarisha usalama wakati wa uwekaji wa alama za mipaka katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo, lililotengwa kwa shughuli za uhifadhi na vyanzo vya maji.

DRC yafunga mipaka yake na Rwanda
Maagizo ya kilimo kwa Ma-DC, Ma-RAC