Kocha wa zamani wa timu ya Taifa ya Misri Hassan Shehata amedai Mshambuliaji Mohamed Salah hajaifanyia chochote timu ya taifa ya nchi hiyo, licha ya kuwa nyota kwenye kikosi cha The Pharaohs.
Kocha huyo mashuhuri, ambaye alishinda Kombe la Mataifa ya Afrika mara tatu mfululizo akiwa na Misri mnamo 2006, 2008 na 2010 anahisi Salah, bado hajatimiza wajibu wake wa kulitumikia taifa.
Amesema Mshambuliaji huyo amekua akipewa sifa lukuki katika vyombo vya habari vya ndani na nje ya Misri, lakini kwake haoni kama ina maana yoyote, kwa sababu hajafikia lengo linalokusudiwa kuisaidia Misri.
“Kiufundi, na ninasikitika kusema hivi, lakini Mohamed Salah hakufanya chochote na timu ya taifa. Alipaswa kufanya vizuri zaidi kuliko hivyo.”
“Ni lazima atoe mengi zaidi anapoichezea nchi yake, nashangaa kuona vyombo vya habari vikimpamba kwa uwezo wake wa kucheza kwa mafanikio makubwa huko Uingereza, lakini ukweli ni kwamba bado katika upande wa The Pharaohs, hajafanya lolote.” amesema Shehata kama alivyonukuliwa na Egypt Independent.
Mo Salah alianza kuitumikia timu ya taifa ya Misri (The Pharaohs) mwaka 2011, baada ya kuzitumikia Timu za Taifa za vijana chini ya umri wa miaka 20 na 23 tangu mwaka 2010.
Akiwa na kikosi cha The Pharaohs, Salah amecheza michezo 85 na kufunga mabao 47, huku akishindwa kuisaidia timu hiyo kutwaa taji lolote tangu alipoanza kuitumikia timu hiyo.
Alikua sehemu ya kikosi cha The Pharaohs, kilichomaliza nafasi ya pili katika Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON’ 2017 na 2021.