Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema anaamini Usajili wachezaji wanaoufanya katika kipindi hiki cha Dirisha la Usajili, utakua jibu sahihi kwa madhaifu yaliyojitokeza msimu uliopita 2021/22.
Simba SC ilishindwa kutetea mataji ya Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ huku ikitolea hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa changamoto ya mikwaju ya Penati dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Try Again amesema wachezaji waliosaini Simba SC na wale wanaendelea kuwafutilia ili kukamilisha taratibu za kutua Msimbazi, wana viwango vizuri na vyenye hadhi ya kurejesha heshima klabuni hapo.
“Yale mapungufu yaliyoonekana msimu uliopita hadi tukashindwa kufanya vizuri na kushindwa kutimiza malengo yetu hasa mashindano ya ndani msimu ujao sidhani kama tunaweza kukutana nayo,”
“Tumekuwa kimya katika usajili kutokana na utulivu wa kutafuta wachezaji wazuri na wenye uwezo ambao tumewafuatilia kwa muda mrefu kama Moses Phiri ili kuongeza makali msimu ujao,”
“Niwahakikishie mashabiki wetu watulie msimu ujao tutakuwa na timu nzuri kutokana na usajili wetu tuliofanya msimu huu pamoja na wale wachezaji ambao tutabaki nao kikosini.”
“Wakati huu tunaendelea kufanya mambo mengine ya kiufundi kwa ajili ya msimu ujao ikiwemo usajili huku tukimuhusisha kocha mpya, Zoran Maki ambaye amekuwa akitoa mchango wake wa mawazo.” amesema Try Again
Simba SC itashiriki Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ msimu ujao 2022/23 ikiwa na lengo la kurejesha heshima ya Ubingwa, huku ikijiwekea mpango wa kufika Nusu Fainali kwenye Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.