Klabu za Zesco United, Nkana Red Devils, Power Dynamos zote za Ligi Kuu Zambia pamoja na FC Saint-Eloi Lupopo inayoshiriki Ligi Kuu DR Congo zinatajwa kuwa kwenye Vita ya kuwania saini ya Mshambuliaji wa Simba SC Chriss Mugalu.
Vita hiyo imeibuka kufuatia tetesi zinazoendelea kuhusu Mshambuliaji huyo kutoka DR Congo kuwa kwenye mpango wa wachezaji ambao huenda wakapewa mkono wa Kwaheri ndani ya Simba SC, katika kipindi hiki cha Dirisha la Usajili kuelekea Msimu Mpya wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Mugalu alipojiunga Simba SC Agosti 2020, akitokea Dynamos alisaini mkataba wa miaka miwili ambao ndani yake ulikuwa na nyongeza ya mwaka mmoja na kuwa mitatu ambao sasa umebaki mmoja.
Mugalu ana mkataba Simba SC lakini kuna mvutano unaoendelea kwani baadhi ya viongozi wanataka waachane naye kutokana na kiwango chake msimu uliopita kuwa chini, huku wengine wakitaka apewe muda zaidi.
Mugalu hakufanya vizuri msimu huu kutokana na kuwa na majeraha, ambapo amemaliza ligi bila kufunga bao hata moja katika michezo aliopata nafasi ya kucheza, tofauti na msimu uliopita akimaliza na mabao 15.
Alipotafutwa Mugalu amesema ameenda kwao kwa ajili ya mapumziko ila bado ana mkataba na Simba SC, unaomalizika msimu ujao huku akidai kama kuna ishu nyingine basi si rasmi.