Mshambuliaji Mpya wa Klabu ya Simba SC Moses Phiri amesema anatarajia ushirikiano mkubwa kutoka kwa Kiungo Clatous Chotta Chama, kufanikisha lengo la kuisaidia timu hiyo msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa.
Phiri ambaye ni mchezaji pekee aliyesajiliwa Simba SC na kutambulishwa kwa Mashabiki na Wanachama katika kipindi hiki cha Dirisha la Usajili, ametoa kauli hiyo kwa kuamini kazi kubwa iliyo mbele yake ni kuisaidia timu hiyo kurejesha heshima ya Ubingwa.
Amesema Chama ni mchezaji pekee anayemfahamu vizuri katika kikosi cha Simba SC kutokana na ushirikiano walioujengwa kwenye timu ya taifa ya Zambia, hivyo anaamini uwepo wake kwenye kikosi cha Msimbazi utamsaidia kwa kiasi kikubwa.
“Nategemea kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa Chama kuelekea msimu ujao, Chama tumecheza wote katika timu ya taifa ya Zambia, namfahamu vyema, ni mchezaji mzuri sana na naamini kwa pamoja tutaipa ubora Simba kwa msimu ujao.” Amesema Phiri
Kuhusu Simba SC kufanya vibaya msimu wa 2021/22, Mshambuliaji huyo amesema jambo hilo halimpi wasiwasi kutokana na kuamini msimu ujao timu hiyo itakua bora na itafanya vizuri kwenye michuano ya ndani na nje ya Tanzania.
“Simba msimu huu nafahamu haijakuwa katika ubora wake lakini naamini kwa msimu ujao kila kitu kitakuwa sawa, tutajitoa kwa uwezo wetu wote tushinde mataji,” amesema mchezaji huyo wa zamani wa Zanazo FC ya Zambia.
Phiri anatarajia kurejea jijini Dar es salaam juma lijalo kujiunga na wachezaji wenzake wa Simba SC, tayari kwa kuanza kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa ambayo rasmi itaanza mwezi Agosti.