Waziri Wa Sanaa, Utamaduni na Michezo Mohamed Mchengerwa amelitaka Shirikihso la Soka nchini ‘TFF’ kutilia mkazo suala la nidhamu katika mchezo wa soka, ili kuleta heshima kati ya Wakuu wanaoendesha mchezo huo na Wadau.
Waziri Mchengerwa alitoa kauli hiyo jana Alhamis (Julai 07), wakati wa hafla ya utoaji Tuzo kwa Timu, Wachezaji, Makocha na Waamuzi waliofanya vizuri kwa msimu wa 2021/22, uliomalizika mwishoni mwa mwezi Juni.
Alisema endapo Nidhamu itadumishwa miongoni mwa viongozi wa wadau, Soka la Tanzania litakua na nafasi kubwa ya kukuwa kwa misingi ya heshima kwa makundi yote bila kujali itikadi.
“Nimepata taarifa kuwa kuna watu hawaheshimu viongozi wao. Niwaombe wachezaji, viongozi na wadau wote wa michezo kuzingatia nidhamu na maadili katika michezo.”
“Bila nidhamu hakuna maendeleo, sitavumilia uvunjifu wa nidhamu katika uongozi wangu” alisema Waziri Mchegerwa
Hata hivyo kauli hiyo ya Waziri Mchengerwa imehusishwa na tukio lililojitokeza Jumamosi (Julai 02) kati ya Msemaji wa Young Africans Haji Manara na Rais wa TFF Wallece Karia, wakati wa mchezo wa Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ mjini Arusha.
Tayari Sekretarieti ya TFF imeshamfungulia mashtaka Haji Manara kwenye Kamati ya Maadili ya Shirikisho hilo, kwa kosa wa kimaadili dhidi ya Rais Wallace Karia, na wkati wowote kesi hiyto itasikilizwa.