Kocha Mkuu wa Simba SC Zoran Manojlovic Maki amesema anaendelea na zoezi la kumfuatilia mchezaji mmoja mmoja ndani ya kikosi cha klabu hiyo, baada ya kukamilisha taratibu za kuajiriwa.

Kocha Maki alitangazwa kuwa Kocha Mkuu Simba SC majuma mawili yaliyopita, akichukua nafasi ya Kocha kutoka nchini Hispania Franco Pablo Martin aliyeondoka klabuni hapo, kufuatia kuvunjwa kwa mkataba wake.

Kocha huyo aliyewahi kuzinoa Primeiro do Agosto ya Angola, Wydad Casablanca ya Morocco na Al Hilal ya Sudan, amesema licha ya ugeni Simba SC, lakini amekuwa akiifuatilia timu hiyo na kuwasoma wachezaji kupitia runinga.

“Nikiwa ndani ya timu nitapata muda wa kufahamu zaidi wachezaji na sifa zao, hii tofauti na wakati huu nimekuwea nawaona kupitia runinga, ila nikiri wengi wao wana vipaji vikubwa na waelewa. Tumaini langu tukiungana, tutafikia malengo ya klabu,” alisema Zoran na kuongeza;

“Baada ya kukubaliana na Simba SC, nimekuwa nikipata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi na kushauriana katika mambo ya kimsingi, haswa yale yanayohusu ufundi.”

“Malengo yangu ni kuhakikisha msimu ujao unakuwa bora tofauti na sasa tulioshindwa kutwaa taji lolote katika mashindano ya ndani, naamini hilo kwa ushirikiano huu linawezekana.” Amesema Kocha huyo kutoka nchii Serbia

Kocha Maki anatarajia kuanza kazi mwezi huu kwa kujiandaa kikosi chake kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

Tanzania kuandaa AFCON 2027
Waziri Mchengerwa ashindilia msumari wa nidhamu TFF