Mtoto wa miaka 17 aliyekuwa akichunga ng’ombe kwenye Hifadhi ya Mkomazi Mkoani Kilimanjaro, amefariki baada ya kupigwa risasi na askari wa Hifadhi hiyo, Julai 6, 2022.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Abdallah Mwaipaya amethibitisha kutokea kifo cha mtoto huyo kilichotokea jana, Julai 9, 2022 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) alikokuwa akipatiwa matibanu.
Mwaipaya alieleza kuwa kwa mujibu wa taarifa za awali, askari wa Hifadhi hiyo walimkamata mtoto huyo kwa kuingiza mifugo hifadhini kinyume cha sheria, lakini aliwaita wenzake ambao walikuja wakiwa wamejihami na mapanga aina ya sime.
“Wale wenzake walikuja na masime jambo ambalo liliwafanya wale askari warushe risasi angani kama 15 hivi kutokana na kwamba wale wafugaji walikuwa wanawafuata,” alisema Mwaipaya.
“Jeshi la polisi linamshikilia askari anayedaiwa kufyatua risasi iliyompata mtoto huyo. Polisi wakishakamilisha uchunguzi wao taratibu nyingine za kisheria zitachukuliwa,” aliongeza.
Akisimulia tukio hilo, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Mkomazi, Emanuel Moirana alisema wananchi waliwavamia askari watano waliokuwa wameshikilia ng’ombe waliokamatwa kwenye hifadhi hiyo. Alieleza kuwa polisi walifyatua risasi angani ili kujihami, na katika purukushani ndipo risasi moja ilimpata mtoto huyo.
Naye Katibu wa Chama cha Wafugaji Wilayani Mwanga, Peter Martine alieleza kuwa baada ya kumkamata mtoto huyo, askari walitaka kuondoka na baadhi ya mifugo, hatua iliyozua purukushani.
“Askari wakawa wanaongea na mchungaji, baada ya muda kidogo wakamtaka atoe sime lake pamoja na simu, vyote akawa ametoa baada ya muda wale askari wakaswaga ng’ombe kuondoka nazo mchungaji kuwakatalia ndipo wakampiga risasi,” alisema Katibu huyo.