Waandamanaji nchini Sri Lanka, wamevamia makazi rasmi ya Rais wa nchi hiyo (Ikulu) na kuchoma moto nyumba ya Waziri Mkuu, wakishinikiza viongozi hao kujiuzulu.
Kwa mujibu wa taarifa ya chombo cha Habari cha Al-Jazeera, viongozi hao hawakuwa katika makazi hayo pindi waandamanaji walipovamia.
Maandamano hayo, yanatokana na harakati za kupinga hali ya uchumi na hatua zinazochukuliwa na Serikali kudhibiti madhara ya mporomoko wa kiuchumi.
Maelfu ya waandamanaji, wameingia katika mitaa ya Mji Mkuu Colombo, na sharti moja tu ili warejeshe hali ya utulivu, nalo ni Rais Rajapaksa kuondoka madarakani.
Kwa mujibu wa Spika wa Bunge la Sri Lanka, Mahinda Yapa Abeywardena amesema Rais, Gotabaya Rajapaksa ametangaza kuwa atajiuzulu na kukabidhi madaraka kwa amani Julai 13, 2022.
Tamko hilo, limesababisha shangwe katika kila kona ya jiji la Colombo, waandamanaji wakiwasha moto kama ishara ya kusherehekea.