Chama cha Wafugaji Wilayani Biharamulo kimemlalamikia Mbunge wa jimbo hilo, Mhandisi Ezra John Chiwelesa juu ya changamoto zinazowakabili ikiwemo kutokutambuliwa na mamlaka za eneo hilo hali inayosababisha migogoro ya mara kwa mara.
Mhandisi Chiwelesa, amekutana na wafugaji wao hii leo Julai 15, 2022 ambapo mbali na kuelezwa tatizo hilo pia wafugaji hao wamesema mbele ya Mbunge wao kuwa wameshindwa kupatiwa eneo la kulisha mifugo yao.
Wamesema, moja ya changamoto yao kubwa katika wilaya hii ni kutotambuliwa na kupewa maeneo ya kufugia na kuchungia mifugo yao, hali itakayosababisha kuondoka kwa migogoro baina yao na wakulima zikiwemo mamlaka za hifadhi za taifa.
“Kuna kero nyingine ya faini ya shilingi laki moja tunayotozwa kwa kila ng’ombe anayekamatwa na taasisi za TANAPA na TFS hii ni kikwazo na sababu inayotufilisi sisi wafugaji,” wamebainisha wanachama wa wafugaji Wilayani humo.
Aidha, Wafugaji hao wameelezea kero nyingine kuwa ni uhaba wa majosho ya kuogeshea mifugo, ambapo wamesema hadi sasa wanatumia yale ya zamani ambayo hayana ubora na yanaweza kusababisha ulemavu kwa mifugo.
Akijibu utatuzi wa kero hizo, Mhandisi Chiwelesa amesema tayari ameongea na Naibu Waziri wa Mifugo, Abdallah Ulega ambaye amemuhakikishia kuwa atazishughulikia kero zao kikamilifu.
“Nimeongea na naibu waziri wa Mifugo Abdallah Ulega na amenihakikishia kushughulikia suala hili kwahiyo tuwe na subira wakati tunangoja hatma ya changamoto zetu,” amesema Mbunge huyo wa Biharamulo.
Kuhusu malalamiko juu ya Wizara ya maliasili na suala la ulipishwaji wa mifugo kwa kiwango hicho, Mhandisi Chiwelesa amesema atayafikisha mahala husika na kuahidi kuyafanyia kazi kwa kuyafuatilia kwa haraka.