Klabu ya Bingwa Tanzania Bara Young Africans imetangaza kuachana na Kiungo Mshambuliaji kutoka DR Congo Chico Ushindi Wakubanza, huku ikiendelea na mazungumzo ya kuvunja mkataba wa Yacouba Sogne.
Young Africans imetangaza maamuzi hayo leo Jumanne (Julai 19), katika Mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika jijini Dar es salaam.
Msemaji wa Klabu hiyo Kongwe katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Haji Sunday Manara amesema kiungo huyo aliyesajiliwa klabuni hapo kwa Mkopo wa Miezi sita akitokea TP Mazembe, hatokua sehemu ya kikosi chao msimu ujao.
Hata hivyo Manara amesema Young Africans ipo katika Mazungumzo ya kusitisha Mkataba na Mshambuliaji kutoka Burkina Faso Yacouba Sogne.
Amesema Maamuzi ya kusitisha mkataba wa Mshambuliaji huyo, yanazingatia Kanuni za Usajili wa Wachezaji wa Kimataifa, ambapo klabu hiyo inapaswa kuwa na Wachezaji 12 pekee.
“Wengi mtajiuliza kwa nini tuna Wachezaji 14 na kanuni zinataka Wachezaji 12 tu, Wachezaji wetu wa kigeni ambao hatutakuwa nao msimu ujao ni Chico Ushindi huku tukiangalia kwa ukaribu hali ya Yacouba Sogne na kufanya makubaliano baina ya pande zote mbili. amesema Haji Manara
Kabla ya kutangazwa kwa Maamuzi hayo, Young Africans ilikua na wachezaji wa Kimataifa 14 ambao ni Fiston Kalala Mayele, Djuma Shaban, Jesus Moloko, Heritier Makambo, Djigui Diara, Khalid Aucho, Yanick Bangala, Stephen Aziz Ki, Lazarous Kambole, Bernard Morisson, Chiko Ushindi, Yacouba Sogna, Joyce Lomalisa na Gael Bigirimana.