Mlinda Lango Chaguo la Kwanza katika kikosi cha Simba SC Aishi Manula ameongeza mkataba mpya wa miaka mitatu ambao utamuwezesha kubaki mitaa ya Msimbazi.
Mapema leo Jumatano (Julai 20), Simba SC imethibitisha taarifa za kumuongeza mkataba Mlinda Lango huyo kupitia Simba APP pamoja na Kurasa za Mitandao ya Kijamii za klabu hiyo.
Akiwa na Simba SC Manula amefanikiwa kuchukua mataji manne ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ mara mbili na kuwa sehemu ya kikosi kilichotinga hatua ya Robo Fainali Afrika mara tatu ngazi ya vilabu.
Kwa mkataba huyo, Manula ambaye amekuwa kwenye kiwango kizuri kwa zaidi ya miaka minne akiwa na Simba SC ataendelea kubakia Msimbazi hadi Mwaka 2025.
Kulikuwa na fununu za kumhusisha mchezaji huyo kutakiwa na vilabu mbalimbali nje ya nchi kutokana na kuonesha kiwango cha hali ya juu hasa katika michezo ya kimataifa kwa msimu uliopita ambapo klabu yake ya Simba SC ilifanikiwa kutinga katika hatua ya Robo fainali ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Kwa sasa Manula yupo kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania ‘TAIFA STARS’ akijiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa Bingwa Afrika ‘CHAN’ dhidi ya Somalia.