Utungwaji wa Sheria ya Uhalifu wa Mtandaoni, umebeba maneno yenye ukakasi na yaliyo hatari zaidi kwa mwanahabari.
Kauli hiyo imetolewa leo Julai 20, 2022 na Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA – TAN), Wakili wa kujitegemea James Marenga, katika semina ya siku moja ya waandishi wa Habari za mtandanoni iliyofanyika Hoteli ya Sapphire Jijini Dar es Salaam.
Amesema, sheria hiyo ina maneno hatari yanayoweza kumuumiza mwandishi kwa kiwango kikubwa, na kutoa angalizo kuwa Sheria hizo zitawaumiza wengi kama hatukauwa na umakini.
Sheria hiyo imeweka baadhi ya maneno ambayo yanaweza kutumiwa vibaya na Mahakama, huku tafsiri ya maneno hayo ikiwa imefichwa ambapo ameyataja baadhi ya maneno yenye mitego katika sheria hiyo kuwa ni pamoja na ‘kwa namna nyingine’ ama ‘kusudio na kinyume cha sheria.’
“Neno kama ‘kwa namna nyingine ama kusudio na kinyume cha sheria,’ ni maneno hatari yanayotumika hasa kuharamisha jambo ambalo sio kosa kisheria na maneno haya unaweza kuyaona kuwa ya kawaida, lakini ni hatari sana,” amefafanua Marenga.
Hata hivyo, amesema kwenye sheria hiyo kuna adhabu zilizowekwa kwa makosa ambayo hayapo wazi kinyume na Ibara ya 13 (6)(C) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sheria hiyo kupitia Kifungu 7 (i)(g) iliyotungwa mwaka 2015, imevuruga uhuru wa faragha ambapo taarifa binafsi za mtu zinaweza kuchukuliwa na polisi kinyume na Ibara ya 16(i) ya Katiba ya Tanzania.
Aidha, ameongeza kuwa, “Sheria hii katika Kifungu cha 50(2)(b) kinaondoa haki ya mtu kukata rufaa kinyume na Ibara ya 13(6)(a) ya Katiba, lakini pia Kifungu cha 38(2)(b) cha sheria hii kinaruhusu usikilizwaji wa shauri mahakamani hata bila muhusika kuwepo na iki ikitolewa, ndio unatafutwa na kufungwa bila kujua kesi yako ilipelekwa Mahakani lini, na kwa kosa gani.