Serikali, imetenga kiasi cha shilingi bilioni 38 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Wilayani Urambo Mkoani Tabora, pamoja na njia ya kusafirisha umeme kutoka Tabora hadi wilayani humo ili kupata umeme wa uhakika.
Waziri wa Nishati January Makamba ameyasema hayo Julai 23, 2022 baada ya kufika katika Kijiji cha Uhuru wilayani Urambo, kwa lengo la kukagua kazi za awali zinazoendelea katika eneo lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupozea umeme.
“Watu wanaongezeka, shughuli zinaongezeka na umeme sasa hautoshelezi mahitaji mapya na Urambo pia ilikuwa ikipata umeme kwa umbali mrefu na kufanya umeme kuja ukiwa mdogo na unaokatika mara kwa mara sasa kwa ujenzi huu hali itakuwa tofauti,” amesema.
Waziri Makamba amesema, hatua za awali zilizochukuliwa na Serikali ni pamoja na kufupisha urefu wa nyaya ili likitokea tatizo popote lisiathiri eneo kubwa na pia kuongeza unene wa nyaya hadi kufikia milimita 100 toka milimita 25.
Amesema, hatua za kudumu zinazochukuliwa na Serikali ni kujenga kituo cha kupoza umeme cha Uhuru kitakachotoa umeme wa uhakika Wilayani humo na kwamba ujenzi wa mradi huo utaanza kutekelezwa mwezi Agosti 2022 na kukamilika mwaka 2023.
Kuhusu fidia ya wananchi waliotoa maeneo ili kutekeleza mradi huo, Makamba amesema, tayari kiasi cha shilingi bilioni 4.3 zimeshatengwa ili kuwalipa fidia wananchi hao na yataanza kufanyika baada ya siku 25.
Katika hatua nyingine, Waziri Makamba amesema Serikali haitaacha kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, kwani ni takwa la Sera ya Nishati ya mwaka 2015 la Serikali kuhakikisha kila mtanzania anapata nishati safi na salama.