Mlinda Lango wa zamani wa Taifa Stars Juma Pondamali ‘Mensah’ ameonyesha matumaini makubwa kwa timu ya Taifa, kuelekea mchezo wa mkondo wa pili wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika dhidi ya Somalia.
Taifa Stars itacheza dhidi Somalia kesho Jumamosi (Julai 30) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikiongoza 1-0, baada ya kuibuka na ushindi huo kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza uliopigwa mwishoni mwa juma lililopita.
Pondamali ambaye pia aliwahi kuwa Kocha wa Makipa wa Taifa Stars amesema ana imani kubwa Kocha Mkuu Kim Poulsen amekiandaa vizuri kikosi chake kwa ajili ya mchezo wa kesho, huku akitambua udhaifu wa Somalia, baada ya kuwaona katika mchezo wa mkondo wa kwanza.
Amesema anaamini lengo kuu la Kocha Poulsen kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza lilikua ni kupata ushindi, na kwa bahati nzuri jambo hilo lilitimia, hivyo kwenye mchezo wa kesho Jumamosi, ana matumaini kuona mbinu nyingine zaidi ya ushindi kwa Taifa Stars kutoka kwa kocha huyo.
“Naamini lengo kuu la Kocha kwenye mchezo wa kwanza lilikua ni ushindi, tunamshukuru Mungu tulishinda kwa bao moja, sasa kesho Jumamosi bado ninaamini kutakua na mbinu zaidi ya kusaka ushindi ili timu iweze kusonga mbele.”
“Somalia walionyesha mchezo wa ajabu sana siku ile, waliweka mtego wa kuzuia na kushambulia kwa kushtukiza, na ndio maana tulipowafunga bao mwanzoni mwa kipindi cha pili walidhihirisha lengo lao la kufunguka kwa mtego, huku wakishambulia kwa nguvu na kushtukiza,”
“Kesho sina shaka tutashinda tu!, kwa sababu hawa Somalia watataka kucheza kwa kufunguka kutokana na hitaji lao la kupindua matokeo, ninaamini kama wakifunguka hapo ndipo tutawapiga vizuri sana,”
“Kocha Kim Poulsen binafsi nimefanya naye kazi, ninajua anachokihitaji katika michezo kama hii, niwatoe hofu watanzania wenzangu kuwa kesho tunakwenda kumaliza mchezo ili tusonge mbele kwenye hii michuano ya CHAN.” amesema Juma Pondamali ‘Menser’.
Katika mchezo wa Mkondo wa kwanza Somalia iliyochagua kucheza michezo yake ya Kimataifa nchini Tanzania ilikua mwenyeji katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, kesho Jumamosi Taifa Stars itakua wenyeji wa mchezo kwenye Uwanja huo.