Waziri wa Nchi ,ofisi ya makamu wa Rais Muungano na mazingira, Selemani Jafo amefanya ziara ya kushitukiza katika soko la Bonanza lililopo jijini Dodoma na kuupongeza uongozi wa soko hilo kwa jitihada za kufanya usafi na kutunza mazingira.
Akiwa katika soko hilo, Wazirn Jafo pia alipata kushiriki zoezi la usafi na kuzungumza na Wafanyabiashara huku akiwapongeza kwa kufanya usafi maeneo yote kwa vitendo bila kushurutishwa.
“Ndugu zangu naomba niwaambie hapa nimeona kitu cha tyofauti sana, nimekuja hapa mnafanya usafi sio kwa kuigiza hongereni sana, nimetembelea maeneo yote kuanzia upande ule wa soko la samaki na nyie ni mfano wa kuigwa na maeneo mengine,” amesema Jafo.
Amesema, wanadodomsa wanatakiwa kulitumia soko hilo la Bonanza kwa ajili ya kununua bidhaa zao kwani lina vigezo stahiki ikiwemo uzingatiaji wa suala la usafi ambao unahimizwa katika maeneo mengine hapa nchini.
Amesema, “Niwaombe maeneo mengine waige mfano wa soko la Bonanza, na Mkurugenzi wetu wa jiji la Dodoma nimuombe jambo hili liendelee katika maeneo mengine mbalimbali tuzingatie hili maana hapa ndiyo makao makuu ya nchi yetu.”
Aidha, Waziri Jafo amefafanua kuwa ili kujilinda na maradhi mbalimbali ni vyema jamii ikatambua umuhimu wa masuala ya usafi na kuzingatia uwepo wa mazingira boya ya kufanyia shughuli mbalimbali hasa ya kibiashara.