Polisi katika Kaunti ya Migori wanachunguza kifo cha mtu mmoja Naftali Nyandera (52), ambaye aliripotiwa kuzimia na kufariki katika nyumba ya kulala wageni aliyokuwa amepanga pamoja na mwenzi wake msichana (24).
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini Kenya, George Kinoti amesema katika ukurasa rasmi wa Twitter kuwa, mtu huyo alianguka na kufariki asubuhi baada ya kulala na mwanamke huyo aliyemzidi miaka 28.
Mwili wa marehemu Naftali Nyandera, uligunduliwa wakati akiwa amelala kwenye kitanda ndani ya nyumba hiyo ya kulala wageni na wakazi wa eneo hilo ambao waliwaita askari Polisi wa Kituo cha Polisi cha Macalder.
Kufuatia tukio hilo, Polisi wa eneo la Nyatike wamemkamata msichana huyo kwa ajili ya mahojiano juu ya tukio hilo la kushangaza.
Mwili wa marehemu kwa sasa umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Migori Level 4, huku chanzo kamili cha kifo kikiwa bado hakijajulikana.
Hili linakuja ikiwa ni miezi michache tangu kutokea kwa tukio jingine Aprili, 2022 ambapo wanaume wawili na mwanamke mmoja walipatikana wakiwa wamekufa katika nyumba ya kulala wageni katika iliyopo eneo la Pipeline jijini Nairobi.
Watatu hao watatu ambao midomo yao ilikutwa imepishana wakiwa wameshikana, haikutambulika wamekutwa na tukio gani ingawa mmoja wao alikuwa akivuja damu mdomoni na puani wakati miili hiyo ilipogunduliwa.
Polisi nchini Kenya walisema tukio hilo bado limeacha kitendawili, na kudai kuwa wanachunguza vifo hivyo ili kubaini kilichotokea kwenye nyumba hiyo ya kulala wageni huku wakidai kuwashuku dhehebu fulani kusababisha tukio hilo.
Kisa kingine, ni kile cha mwezi mmoja (Juni, 2022), baada ya katibu wa shirika la Ford Kenya wa eneo la Bungoma, Moses Nabibya kupatikana amefariki ndani ya nyumba ya kulala wageni huko Webuye, ambapo pia mwanammke mmoja (25) alishikiliwa na Polisi kwa mahojiano.