Kama nilivyotarajia, sinema ya Haji Manara dhidi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au kwa maneno mengine, Rais, Wallace Karia, limeibuka tena mwishoni mwa wiki baada ya msemaji huyo wa Yanga, aliyefungiwa wa kuibuka kwenye Tamasha la Kilele cha Wiki ya Mwananchi akiwa kama mshereheshaji.

Kwa wale wanaokurupuka wakati wa matukio, wanaweza kusema naandika hii kwa sababu ya Haji Manara.

Lakini kwa wanaofuatilia, hili ni andiko langu la karibu tisa au kumi kuhusu uendeshaji wa mashauri unaofanywa na Kamati ya Maadili na ya Nidhamu kinyume na utamaduni wa mpira.

Kama nilivyotarajia, sinema ya Haji Manara dhidi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au kwa maneno mengine, Rais, Wallace Karia, limeibuka tena mwishoni mwa wiki baada ya msemaji huyo wa Yanga, aliyefungiwa wa kuibuka kwenye Tamasha la Kilele cha Wiki ya Mwananchi akiwa kama mshereheshaji.

Tukio hilo likanogeshwa zaidi na kasi ya sekretarieti kumshtaki kesho yake asubuhi, kana kwamba ilishajiandaa kwa tukio hilo na haikuhitaji muda wa kulitafakari kwanza.

Kama ilivyokuwa siku ile kule Arusha, ndivyo ilivyokuwa Jumapili asubuhi kwamba sekretarieti imerudi tena kwa kasi mbele ya Kamati ya Maadili, pengine ikijua haitaitwa kuhojiwa na kama uamuzi upo tayari ulikuwa unasubiri kosa.

Kwangu mimi suala si Haji kufanya kosa au kutofanya. Kwangu ni jinsi gani kanuni za maadili zinavyotumiwa kwa njia ambayo ni kama ya kukomoa; ukishtakiwa huchomoki.

Ila kilicho dhahiri ni kwamba ukiukwaji wa maadili unaongezeka na pengine TFF inakuwa ndio mwanachama pekee wa Fifa aliyefungiwa wengi ndani ya muda mfupi.

Hapo ndipo unapohoji tatizo ni wakosaji, kamati, kanuni au matumizi yake?

Kuna watu wanashabikia adhabu hizo kwa fikra kwamba zitairejesha familia ya mpira katika maadili kwa sababu Rais wa zamani wa TFF, Leodger Tenga alikuwa softi, lakini hawaangalii utamaduni wa mpira unasemaje.

Kuna watu wanashangilia kwa kumuangalia Haji, lakini hawaangalii mpira katika picha kubwa, hasa soka la kulipwa ambalo linazingatia kuwa yeyote anayejihusisha nalo, analitegemea kama njia kuu ya kumuwezesha kuiishi na soka la ridhaa ambalo washiriki wana ajira nyingine huku mpira ukiwa ziada.

Ile video ya lile tukio lililosababisha Haji afungiwe bado inaniambia kuwa kulikuwa na pande mbili zinazozana. Mashtaka ya TFF pekee hayatoshi kumtia Haji hatiani. Wakati mpira unajiondoa katika mahakama za kawaida, ulilenga kutumia vyombo vyake vya haki ili kutafuta ukweli na kuushughulikia.

Katika mahakama za kawaida shauri linaweza kuishia hatua za awali kwa sababu kiapo kilikosewa, ama mahakama haina mamlaka ya kusikiliza shauri hili, au jina la mshtakiwa lilikosewa.

Na kibaya zaidi na mwenendo wake wa mashauri; shauri linaweza kuchukua miezi hadi miaka kumalizika.

Na shauri hilo linaweza kuambatana na amri ya muda ya mahakama kuzuia shughuli nyingine zisiendelee hadi hukumu itakapotolewa.

Kwa mfano klabu imeshtakiwa kwamba haikumsajili Bernard Morrison kihalali halafu iliyomsajili ikaomba amri ya mahakama kuzuia mechi zake zote hadi suala la mchezaji wake litakapotolewa uamuzi. Hapo kusingekuwa na ligi!

Kwa hiyo, vyombo vya haki vya mpira vinalenga kutafuta ukweli na si mbinu za kisheria kukwamisha shauri na pili kuhakikisha mambo yake yanakwenda kwa kasi inayolingana na utamaduni wa soka.

Ni dhahiri Kamati ya Maadili ilitakiwa ipate ukweli wote kuhusu sakata la Haji-Karia.

Na uzuri ni kwamba kanuni zinaipa mamlaka kamati kufanya uchunguzi wa jambo kabla ya kushtaki. Kwa hiyo, sioni ajabu kwamba Haji anajiona hakutendewa haki, licha ya kuomba radhi kwa kuzozana na rais wa TFF, kitu ambacho si kosa kikanuni bali ni uungwana.

Kwa kuwa Haji anajiona hakutendewa haki na ukweli usemaji wa Yanga kwa sasa ndio ajira yake, atatafuta kila mbinu aiangushe TFF ili aendelee kujipatia riziki katika mchezo huu.

Utamaduni wa mpira wa kulipwa ni kupiga faini wakosaji na kufungia pale panapoonekana kuna umuhimu mkubwa.

Wakati Rais Jakaya Kikwete anahutubia wanamichezo siku Kombe la Dunia lilipokuja kwa mara ya kwanza Tanzania, alisisitiza sana umuhimu wa TFF kuachana na adhabu za kufungia watu badala yake ianzishe faini na kupunguza urefu wa adhabu.

Yaani Mchezaji, Juma Nyoso apigwe faini na adhabu ya mechi nne tu kwa sababu ni kosa la kinidhamu.

Hata Rio Fernand alipokwepa vipimo vya dawa za kusisimua misuli, alifungiwa miezi minane tu. Kosa la matumizi ya dawa hizo ni kubwa sana kwa wachezaji, pamoja na yale ya kupanga matokeo. Iweje aliyefanya kosa ndani ya dakika tisini aadhibiwe kuliko yule aliyekwepa kuchukuliwa vipimo?

Kocha Mbwana Makatta alifungiwa miaka mitano eti kwa kuchochea wachezaji wagomee mchezo kutokana na kutokuwepo uwanjani kwa gari la wagonjwa kama kanuni zinavyotaka.

Iweje aliyetaka kanuni ziheshimiwe aadhibiwe halafu ambaye alikiuka kanuni angalau asionywe? Kumbuka yule kipa wa Arusha FC, Nazir Mussa Mchomba alifariki kwa kucheleweshewa huduma ya kwanza katika mechi ligi jijini Mbeya baada ya daluga la Kenneth Pesambili wa 44 KJ kulikata koromeo lake.

Sasa unajiuliza iweje aliyeshindwa kuhakikisha gari linakuwepo uwanjani asipewe hata onyo?

Sijui kama Kamati ya Maadili ilihoji haya katika kutafuta ukweli wa sakata la Makatta. Sekretarieti ni mhusika katika uandaaji wa mechi za Ligi Kuu na hata mechi nyingine za kirafiki za mikoa, wilaya au klabu kutokana na dhamana yake kitaifa.

Hapo ndipo unapokutana na sakata jipya la Haji. TFF imechukua jukumu la kuhusika hadi katika mchezo wa kirafiki wa Yanga pamoja na sherehe zake.

Haikumbuki ilihusika katika mchezo wa Namungo na Dodoma Jiji. Lakini leo inahusika katika kujua maofisa wa mechi ya tamasha!

Mtu mmoja kaandika mtandaoni kuwa ni kweli TFF inahusika katika mechi ya Yanga na Vipers ya Uganda, lakini inatakiwa ihusike hadi katika sherehe za Tamasha la Wiki ya Mwananchi? Au kwa sababu lilifanyika kabla ya mchezo?

Kufungiwa kushiriki katika shughuli zinazohusiana na soka maana yake nini? Kufanya shughuli tofauti na mpira wa miguu? Usichambue soka kama Shaffih Dauda ambaye anachambua soka huku akiwa na adhabu ya kutojihusisha na mchezo huu?

Kwamba Yanga ikimpa Haji kazi ya kuuza jezi, TFF itamzuia kwa sababu jezi ni za soka? Yanga ikiwa na sherehe pale Jangwani, Haji asishiriki? Au kukiwa na timu ya Bonanza huko, Haji haruhusiwi kuwa msemaji? Nini maana ya shughuli zinazohusiana na soka?

Ni shughuli ambazo mwishoni zitaihusisha TFF? Nadhani ni pale TFF itakapokataa kitu chochote kinachofanywa na Haji kwa niaba ya Yanga kuhusu mpira wa miguu. Au pale Haji atakapofanya shughuli rasmi ya kazi yake ya usemaji kwa niaba ya Yanga, basi atahesabika kama amekiuka adhabu. Sidhani kama kutambulisha wachezaji imo katika orodha shughuli za TFF. Atakapotoa taarifa rasmi kuhusu Yanga kwenda kwa familia ya soka au kwa TFF, basi hapo atakuwa amekiuka adhabu.

Vipi akilipwa mshahara?

Ndio, TFF haitamruhusu kushiriki shughuli kama semina, mafunzo, mikutano yake na shughuli nyingine zinazoandaliwa na wanachama wake. Haji aliadhibiwa kama mwajiriwa wa Yanga na si kama shabiki ambaye huweza kuzuiwa asiingie hata uwanjani.

Kwa maana nyingine, Haji ameipa changamoto TFF kuwa kuna haja ya kwenda mbali zaidi katika kushughulikia maadili na si kutoa hizi adhabu za jumlajumla ambazo zitaifanya iingie katika kazi ya kutafsiri kilichoamuliwa.

Kwangu mimi, kama nilivyoeleza katika makala za awali, maamuzi ya hii kamati na mchakato wa mashauri yanaibua hoja kwamba kunahitajika kuangalia zaidi uwasilishaji wa mashauri, wahusika na pia kurudi kwenye kanuni za maadili za Fifa kuona jinsi adhabu zinavyotolewa.

Kama Fifa iliunda investigatory chamber (kitengo cha uchunguzi) na adjudicatory chamber (kiitengo cha mashtaka) ndani ya Kamati ya Maadili, kwanini sekretarieti iendelee kuwa mshtaki? Uchunguzi hufanywa na chombo tofauti na sekretarieti ya Fifa na mashtaka huendeshwa kwingine.

Wakati utata unapokuwa mkubwa kuhusu haki na adhabu kama ilivyo sasa, kuna umuhimu wa TFF kwenda mbali zaidi katika kuimarisha vyombo vyake ili wanafamilia wawe na imani navyo.

Via MWANASPOTI.

Bingwa wa CAF SUPER LEAGUE kulamba dola milioni 100
Rais wa FIFA, CAF kuitazama Kariakoo Derby Jumamosi