Kukatika mara kwa mara kwa umeme, ambako kumeyakumba baadhi ya maeneo nchini Uganda ikiwemo mji mkuu wake Kampala, kumeulazimisha utawala wa Rais Yoweri Museveni kufanya makubaliano ya dharura na nchi ya Kenya.
Waziri wa Nishati wa Uganda, Ruth Nankabirwa Ssentamu, ametangaza kuwa Kenya imekubali kusafirisha umeme kwenda nchini humo na itawalazimu kununua megawati 60 kutoka nchi hiyo ya jirani ili kuondokana na adha inayowakabili.
Mpango huo unakuja baada ya mafuriko kukikumba kiwanda cha mashine za kuzalisha umeme Isimba nchini Uganda, kilicho na megawati 183 wiki jana, na kulazimisha kuzimwa kwa mitambo yake ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Ssentamu ameonya kuwa, baadhi ya maeneo ya Uganda hasa yaliyo kando ya njia za usambazaji wa uokoaji wa Bwawa la Isimba, yataendelea kupata umeme wa hapa na pale.
“Tulilazimika kukusanya hatua ili tusipate shida kubwa ya kumwaga mzigo (Kusambaza mahitaji ya nishati ya umeme katika vyanzo vingi vya nishati ili kupunguza msongo wa nishati ya msingi),” alisema Ssentamu.
Kuhusu hatua ya Uganda kununua umeme kutoka Kenya, Ssentamu amesema nchi hizo mbili zilikuwa na makubaliano kuhusu biashara ya umeme na watailipa Kenya wakati wowote Bwawa la Isimba litakaporejesha huduma zake.
Mafuriko katika bwawa hilo lililoanzishwa miaka mitatu tu iliyopita, yalitokana na makosa ya kibinadamu kuvamia kingo za mradi huo, ingawa hakutoa maelezo zaidi juu ya mgogoro huo.
Hata hivyo, mvua zinazoendelea kunyesha nchini Uganda zinakuja mara baada ya ukame wa muda mrefu katika maeneo mengi ya nchi hiyo, ambayo iliacha maeneo mengi kuwa makame na mazao mashambani kuungua.
Zaidi ya watu 300,000, waliathiriwa na mafuriko na maporomoko ya ardhi Mashariki mwa Uganda hasa maeneo ya Bundibugyo Magharibi, huku ikikadiriwa kuwa watu 65,000 pia walilazimika kuyakimbia makazi yao.