Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi chini ya Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ Nassoro Hamduni ametetea maamuzi ya Mwamuzi Elly Sasii, aliyechezesha mchezo wa Ngao ya Jamii kati ya Simba SC dhidi ya Young Africans, Jumamosi (Agosti 13), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Mwamuzi Sasii analalamikiwa na baadhi ya Mashabiki wa Soka nchini kwa kushindwa kumuonyesha Kadi Nyekundu Beki wa Simba SC Henock Inonga, baada ya kumchezea rafu kiungo wa Young Africans Abubakar Salum ‘Sure Boy’.
Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF Nassoro Hamduni amesema anashangazwa kuona mjadala mzito dhidi ya Mwamuzi Sasii kwenye mitandao ya Kijamii na katika baadhi ya vyombo vya habari, unaohusu Maamuzi aliyoyachukua kwa kumuonyesha Kadi ye Njao Inonga kwa kosa alilolifanya dhidi ya Sure Boy.
Amesema Mwamuzi Sasii alikua sahihi kufanya hivyo, na ameshauri kuwa Wadau wa Soka la Bongo wanapaswa kuheshimu kazi ya Uamuzi ambayo mara kadhaa imekua ikiwekewa mijadala mbalimbali kwa lengo la kukosoa.
Mwenyekiti Hamduni amesisitiza kuwa umefika wakati sasa Waamuzi wa Soka nchini wanapaswa kuachwa wafanye kazi yao, na wasiingiliwe katika maamuzi, huku akiwataka Wadau wa Soka la Bongo wasitegemee maamuzi ya mezani.
“Imekua kawaida sana kwa wadau wa Soka nchini kulalamika dhidi ya Waamuzi wanaochezesha, ni muda sasa wakajifunza kuacha hiyo tabia kwa sababu kazi ya uamuzi ni kazi kama kazi nyingine ambazo zinafanywa Kitaaluma na Weledi.”
“Sasii alikua sahihi kumuonyesha kadi ya Njano Inongo kwa sababu yeye alijiridhisha na kuona adhabu hiyo ilimfaa mchezaji huyo, iweje wanakuja watu na kuhoji tena kwa kukosoa maamuzi aliyoyafanya, kwangu mimi naamini Mwamuzi alikua sahihi kufanya vile,”
“Tunapaswa kuheshimu hii kazi na kuiona kama kazi nyingine, soka ni mchezo wa wazi na kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni yake, lakini yanatakiwa kuwa ndani ya mipango ya kujenga na sio kukosoa kama wanavyofanya baadi ya watu, pia wasitegemee maamuzi ya mezani.” amesema Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi ya TFF Nassoro Hamduni