Raila Amolo Odinga mwenye umri wa miaka 77, mwanasiasa mkongwe wa Kenya ambaye amejaribu kuwa rais wa nchi hiyo mara tano, na katika nafasi nne aliibuka katika nafasi ya pili licha ya umaarufu mkubwa alionao.

Raila amehudumu kama Waziri Mkuu wa Kenya Kwa mwaka 2008 hadi 2013 kwenye serikali ya mseto iliyoundwa baada ya ghasia za uchaguzi wa 2007, wakati huo marehemu Mwai Kibaki alitangazwa mshindi.

Raila Odinga na Mwai Kibaki. Picha na UGC, Chanzo Getty Images.

Ni mfanyabiashara mkubwa na alihudumu kama Mbunge wa Lang’ata tangu 1992 hadi Machi 2013 akiendelea na harakati zake za kisiasa kila alipotaka kuwania Urais wa Nchi hiyo kabla ya kuingizwa kwenye muungano wa BBI.

Raila alishindwa kwenye uchaguzi mara mbili na Rais Uhuru Kenyatta miaka ya 2013 na 2017, na pia kushindwa na Naibu Rais William Ruto kwenye uchaguzi huu wa 2022.

Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amekuwa katika siasa kwa miongo minne kuanzia mwaka 1982 hadi sasa mwaka wa 2022 ambapo ni takriban miaka 40.

Katika harakati za Urais, Raila alishindwa na Daniel Arap Moi na Mwai Kibaki.

Raila Odinga na Daniel Mo. Chanzo: The standard

Mwanzo aliwania urais mwaka 1997 kwa tiketi ya chama cha NDP akishika nafasi ya tatu nyuma ya Daniel Moi wa KANU na Mwai Kibaki wa DP.

Mwaka 2002, Raila alimuunga mkono mgombea wa Narc Mwai Kibaki aliyeibuka mshindi na kumbwaga Uhuru Kenyatta wa KANU.

Baada ya kukosana na Kibaki, Raila aliwania urais kwa tiketi ya chama cha ODM mwaka 2007 lakini ashindwa tena na Kibaki ambaye alitumia chama cha PNU.

Raila aligombea akiwa na Kalonzo Musyoka kama mgombea mwenza lakini wakashindwa na Uhuru Kenyatta na mgombea mwenza wake William Ruto mwaka 2013 na 2017.

Raila Odinga na Kalonzo Musyoka.

Mwaka 2022, imekuwa ni mara ya tano Raila kuwania urais, kwa wakati huu akiwa na Martha Karua kama mgombea mwenza dhidi ya William Ruto na Rigathi Gachagua wa chama cha UDA.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa Jumatatu, Agosti 15, na mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati Raila alishindwa tena.

Lakini ni nini kinafuata kwa Raila baada ya miaka 40 ya siasa zisizoshinda?

Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Raila kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani, Mwaka 2013 alifika katika mahakama ya upeo kupinga ushindi wa Uhuru Kenyatta, lakini rufaa hiyo ikatupwa nje huku rufaa yake ya 2017 ikikubaliwa na ushindi wa Uhuru kufutwa.

Raila Odinga na Uhuru Kenyatta

Endapo akijaaliwa afya na Nguvu, Raila ana nafasi ya kugombea urais kwa mara nyingine katika uchaguzi wa mwaka 2027 ambayo itakuwa ya sita na atakuwa na umri wa miaka 82.

Kando ya changamoto ya umri, Raila pia atakuwa na shughulki pevu ya kumng’oa madarakani Ruto iwapo ataapishwa kwani atalenga kupata muhula wa pili kabla ya kuachilia mamlaka.

Kustaafu siasa kuna uwezekano mkubwa pia kutokana na umri wake mkubwa na kuvunjwa moyo ambako amepata kila mara katika siasa za Kenya.

Wiki chache kabla ya uchaguzi wa 2022, kaka yake mkubwa Oburu Odinga alisema kuwa wangemshauri Raila kustaafu na kujishughulisha na kazi nyingine iwapo atapoteza uchaguzi wa urais.

“Tuna Imani kama familia kuwa atashinda lakini iwapo atapoteza uchaguzi huu, sasa tutamshauri kuondoka na kujishughulisha na kitu kingine,” Oburu alinukuliwa na gazeti la the Star.

Lakini pamoja na yote hayo yanayoendelea kwa Raila Amolo Odinga, wapo ambao wamepata moyo wa huruma na kuhamasisha kumuombea.

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko ametuma jumble katika mtandao wake wa twitter ukiashiria kumuonea huruma Raila kwa kushindwa urais mara tano, miaka ya 1997, 2007, 2013, 2017 na 2022.

“Wakenya wapendwa, kwa heshima ya nchi hii na rafiki yangu Raila Odinga, na licha ya mambo yaliyotokea awali na hivi sasa, nadhani muda umewadia kwa taifa kumuweka Baba kwa maombi,” Sonko aliandika ujumbe huo kwenye Twitter siku ya Jumatano.

Ajali zauwa zaidi ya 30 ndani ya mwezi mmoja
AZAKI Pemba yaweka mikakati kuongeza uwajibikaji Taasisi za Umma