Zaidi ya watu 30 wamepoteza maisha ndani ya mwezi mmoja kutokana na ajali za Barabarani katika Mikoani miwili nchini ikiwemo na Singida, zilizosababishwa na vyanzo mbalimbali ikiwemo mwendokasi na makoya ya kibinadamu.
Ajali hizo, ni pamoja na ile iliyotokea Agosti 8, 2022 ambapo watu 22 walipoteza maisha Mkoani Shinyanga, Agosti 9, 2022 watu sita wakipoteza maisha Wilayani Nkalama na Agosti 17, 2022 watu watano wakipoteza maisha wilayani Manyoni kufuatia basi la Kampuni ya Tanzanite kupasuka tairi na kupinduka Mkoani Singida.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Singida, Stella Mutabihirwa akiongea na vyombo vya Habari juu ya matukio ya ajali Mkoani humo amesema ajali ya Agosti 17, 2022 iliyohusisha basi la Tanzanite, lililokuwa likitokea Mkoani Mwanza kuelekea jijini Dar es Salaam na kuuwa watu watano ilisababishwa na uzembe wa Dereva.
Amesema watu wanne walifariki papo hapo, huku abiria waliokuwa ndani ya basi hilo wakisema wakiwa eneo la Kijiji cha Mbwasa Wilayani Manyoni lilikuwa likiendeshwa kwa mwendokasi na Dereva wa basi kushindwa kulimudu kisha likapoteza mwelekeo na alikimbia mara baada ya ajali kutokea.
Kamanda Mutabihirwa, amesema watu 15 walijeruhiwa katika ajali hiyo na kudai kuwa kuwasihi madereva wafuate sheria za barabarani ikiwemo kuchukua tahadhari.