Joto la Mpambano wa Mzunguuko wa Tatu wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Mabingwa watetezi Young Africans dhidi ya Azam FC limeanza kupanda huku kauli ya ‘Kisasi’ ikichomoza.
Azam FC ilipoteza michezo yote miwili dhidi ya Young Africans msimu uliopita 2021/22, hali ambayo ilichukuliwa kuwa Matajiri hao wa Dar es salaam hawawezi kutamba mbele ya Wananchi.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasilino ya Azam FC Thabit Zakaria ‘ZakaZakazi’ amesema Uongozi umejipanga kikamilifu kuhakikisha mambo yanawanyookea katika mchezo huo, ambao utapigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Septemba 06.
‘Zakazakazi’ amesema wanatambua msimu uliopita mambo yalikua magumu upande wao baada ya kupoteza michezo yote miwili, lakini msimu huu hawatakubali kuona hali hiyo ikijirudia tena, ili hali wana kikosi kizuri na kilicho bora.
Amesema ‘Kikasi’ kinapaswa kulipwa ili kuweka mambo sawa na kurejesha heshima mjini, kwa sababu Nia, Dhamira na Mipango wanayo.
“Kuhusu mchezo uliopita ni kama makosa yalitokea, lakini tulikuwa bora zaidi kwenye takwimu, tulikuwa juu kimpira, lakini soka ni mchezo wa makosa, utakapokosea mpinzani anatumia makosa yako kukuadhibu”
“Msimu huu tumejipanga kupambana bila kuchoka, hatutakubali kupoteza tena kama ilivyokua msimu uliopita, ninaamini utakua mchezo wenye upinzani mkubwa, na mipango tuliojiwekea nina uhakika mambo yatatunyookea na ‘Kisasi’ kitalipwa.” amesema ZakaZakazi
Katika msimamo wa Ligi Kuu hadi sasa Azam FC ipo nafasi ya sita baada ya kucheza michezo miwili, ikishinda dhidi ya Kegara Sugar na kutoka sare dhidi ya Geita Gold FC.
Young Africans ipo nafasi ya pili ikiwa na alama sita, baada ya kucheza michezo miwili ugenini, ikishinda yote dhidi ya Polisi Tanzania na Coastal Union.