Baada ya kuanza vibaya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23, Kocha Mkuu wa Ihefu FC Zuberi Katwila ametoa kauli ya matumaini kwa Mashabiki wa klabu hiyo yenye Maskani yake Makuu mjini Mbarari Mkoani Mbeya.

Ihefu FC ilianza Ligi Kuu kwa kupoteza 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting na Kasumba hiyo iliendelea katika mchezo wa Mzunguuko wa Pili dhidi ya Namungo FC.

Kocha Kawila amesema ana matarajio makubwa na kikosi chake kufanya vizuri katika michezo ijayo kwa kuwa atakitumia kipindi hiki cha mapumziko ya kupisha Kalenda ya FIFA, kujifua zaidi ikiwamo kutengeneza muunganiko mzuri wa kikosi chake.

Amesema, tatizo kubwa la kutofanya vizuri katika michezo miwili iliyopita ni kwa sababu ya kukosa muda wa maandalizi ya msimu mpya baada ya kufanya usajili wa kuongeza wachezaji wengi wapya.

“Nakiri kweli hatujakuwa na muunganiko mzuri, lakini haya mapumziko ya ligi kusimama, tutatumia kufanyia kazi yale tuliyoyaona katika michezo miwili na Ligi Kuu ikirejea tutakuwa imara zaidi,” amesema Katwila.

Amesema usajili wao wamefanya kulingana na mahitaji ya timu na matarajio makubwa ya kufanya vizuri katika ligi msimu huu kuepuka kilichowatokea msimu walipanda Ligi Kuu na kushuka Daraja.

Katwila, amesema kazi kubwa anayoifanya ni kukinoa kikosi chake hususan safu ya ulinzi na umakini kwa washambuliaji ili mechi ijayo wakatafute matokeo chanya kwa kuondoka na alama tatu.

Mchezo ujao kwa Ihefu FC, itaifuata Mtibwa Sugar Septemba 7, mwaka huu, katika Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.

Waliokufa kwa Uviko-19 wafikia Milioni 1
Walioiba mafuta watakiwa kuyarejesha haraka