Kocha Mkuu wa Simba Queens, Sebastian Nkoma, amefunguka na kudai kuwa mshambuliaji wake, Opa Clement bado yuko vizuri na muda si mrefu atarejea katika ubora wake wa kufumania nyavu.
Nkoma amesema, Opa bado ana uwezo wa kufunga na hajashuka kiwango ila katika michuano hiyo alimpa majukumu mengine.
Amesema, kitendo cha wapinzani kuelekeza akili yao katika kumkaba sana Opa, kiliwafanya wachezaji wengine kupata nafasi ya kufunga.
“Opa hajashuka kiwango, nina imani kutofunga katika michezo mitatu tuliyocheza ni kutokana na wapinzani wetu kumfikiria zaidi yeye na kumkaba, hivyo tukatumia nafasi hiyo kwa wengine kufunga.
“Awali, ilikuwa ngumu baada ya kuona mechi mbili hajafunga ilimtoa mchezoni, nilikaa naye na kumweleza kwamba anatakiwa asikate tamaa na kutakiwa kuachia mpira anapokuwa amekabwa na kutoa nafasi kwa wengine, kufunga jambo ambalo alinielewa,” amesema kocha huyo.
Kuhusu usajili wao mpya, Vivian Corazone, Nkoma amesema ni mchezaji mzuri kwenye eneo ya kiungo, ulinzi hususan katika kugombea mipira.
“Kuhusu Teopister Situma, bado yuko chini (Slow) ni mshambuliaji wa kweli, ninatakiwa kupata muda wa kumwandaa, matarajio yangu atakuwa bora zaidi katika muda mfupi kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania,” amesema.