Tume ya Mishahara na Marupurupu nchini Kenya, (SRC) imeeleza mbinu iliyotumia kufikia ufutaji wa posho za vikao pamoja na ruzuku ya magari na usafiri wa Wabunge ulioanza kutekelezwa kuanzia Agosti 9, 2022.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa SRC Lyn Mengich, tume iliangalia malipo ya maafisa wa serikali kutoka kwa kanuni za usawa na haki kwani wabunge walikuwa wakilipwa mshahara wa juu zaidi ya mahitaji yao ya malipo ya ofisi.
Amesema hayo wakati wa mahojiano na kituo cha runinga cha Citizen, ambapo ameeleza kwamba wabunge walikuwa wakipata malipo sawa na ya Gavana, ikiwa marupurupu ya vikao vya mikutano ya kamati na marupurupu ya vikao vya jumla yatahesabiwa.
Mengich amebainisha kuwa mshahara wa kimsingi wa mbunge kama inavyoelekezwa katika daraja lao la malipo ni Ksh 710,000 lakini pamoja na marupurupu hayo wanaishia kupokea Ksh 920,000 kila mwezi.
“Upangaji wa sasa wa Wabunge ulipandishwa daraja hadi daraja tunaloliita F1 ambalo ni sawa na daraja la PS,” amesema Mengich.
“Leo malipo ya daraja la F1 ni Ksh 765,000 lakini kwa mbunge ni zaidi ya hapo kwa sababu malipo yao ni Ksh 710,000 kabla hatujaongeza marupurupu ya vikao vya kamati ambayo ni karibu Ksh 120,000.
Hii yote ni karibu Ksh 830,000 ambayo ni juu ya mshahara uliowekwa kwa jukumu la F1, “ameeleza
“Na hiyo ni hata kabla ya kuongeza posho ya kikao cha jumla ambayo itawawezesha kupata Ksh 920,000 ambayo inamaanisha utakuwa ukimlipa mbunge sawa na Katibu wa Baraza la Mawaziri au Gavana.”
Bosi huyo wa SRC pia amebainisha kuwa kukomeshwa kutawaokoa walipa ushuru kutokana na kulipa ushuru wa juu kwani malipo ya marekebisho ya marupurupu yataongeza akiba ya jumla ya Ksh 8.2 bilioni kwa Bunge la Kitaifa na Bunge la Kaunti katika akiba ya kipindi cha miaka 5 ya serikali.
Haya yanajiri huku kukiwa na vitisho vya wabunge katika Bunge la 13 kuivunja tume hiyo huku mabadiliko hayo yakipangwa kuanza kutekelezwa.