Nahodha na Mshambuliaji wa kikosi cha Timu ya Taifa ya Uganda ‘The Cranes’, Milton Karisa amefunguka kuelekea mchezo wa Mkondo wa Pili wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ dhidi ya Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Miamba hiyo ya Afrika Mashariki itakutana kesho katika Uwanja wa St Marry’s mjini Kampala mishale ya jioni, huku wenyeji Uganda wakiwa mbele kwa bao moja, walilolipata kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa Jumapili (Agosti 28), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Karisa ambaye alikua sehemu ya kikosi kilichoikabili Stars jijini Dar es salaam, amesema wapo tayarti kwa mchezo huo na wana matumaini ya kuendeleza kipigo kwa Tanzania na kisha kufuzu kwenye Fainali za ‘CHAN’

Akizungumza katika Mkutano maalum na Waandishi wa Habari uliofanyika mjini Kampala mchana huu, mshambuliaji huyo wa klabu ya Vipers SC amesema wamejiandaa vya kutosha na wanajua wapi ulipo udhaifu wa Taifa Stars.

“Tumejiandaa vizuri kwa ajili ya mchezo wetu (dhidi ya Tanzania) na tupo tayari kupambania kupata matokeo” amesema Karisa.

Mbali na mipango ya kusaka ushindi dhidi ya Taifa Stars katika mchezo wa Kesho, sare ya aina yoyote itakivusha kikosi cha Uganda na kukata Tiketi ya kucheza Fainali za ‘CHAN’.

Taifa Stars itatakiwa kusaka ushindi wa zaidi ya bao moja dhidi ya Uganda, ili kukata tiketi ya kushiriki Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ zitakazounguruma nchini Algeria mwaka 2023.

Kenya: Wakili atoa ushahidi wa Mvenezuela kushiriki uchaguzi
Singida Big Stars yathibitisha kumtema Mwendwa