Wakandarasi wa ujenzi wa mradi wa barabara ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma, wametakiwa kuongeza kasi ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati na kwa viwango.
Wito huo umetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mkoani Dodoma, wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara ya mzunguko wa nje wa jiji hilo lililopo katikati ya makao makuu ya nchi.
Amesema, “Kazi inaendela vizuri, tunataka kazi ikamilike ikiwezekana hata kabla ya muda, Rais Samia Suluhu Hassan anatekeleza miradi hii ili iwanufaishe Watanzania, hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunasimamia na inakamilika kwa viwango na wakati.”
Aidha, amewataka Wahandisi Wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha wanasimamia kikamilifu wakandarasi ili barabara hiyo ili iweze kujengwa kwa viwango vilivyokubaliwa kwenye mkataba wa ujenzi.
Akizungumza na watanzania walioajiriwa katika mradi huo, Majaliwa amewataka wawe walinzi wa vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi na wahakikishe vifaa vinabaki salama “Pambaneni na wote wenye nia ya kuiba vifaa hivi, tunataka tupate barabara yenye viwango”
Waziri Mkuu, pia ametaka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kuweka utaratibu wa kuwaweka pamoja vijana ambao wanashiriki kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali nchini ili waweze kutumika zaidi kwenye makampuni ya ujenzi ya wazawa.
Awali, Kaimu Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Salome Kabunda alisema pamoja na mradi huo kusaidia kupunguza msongamano wa magari jiji la Dodoma pindi utakapokamilika, pia umesaidia kutoa ajira kwa wazawa zaidi ya 800.
Ameongeza kuwa sehemu ya kwanza ya ujenzi wa barabara hiyo kutoka Nala-Veyula-Mtumba hadi bandari kavu ya Ihumwa (Km 52.5) unaojengwa kwa muda wa miezi 39, utagharimu shilingi bilioni 100.
Ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilimota 112.3, unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).