Baada ya kuonesha Soka safi katika Michezo mitatu ya Kimataifa ya Kirafiki wakati wa mapumziko ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Beki Mzawa Nassoro Kapama amekuwa sehemu ya wachezaji waliomkosha Kocha Mkuu wa Simba SC Zoran Maki.
Kapama alionesha kiwango kizuri wakati wa mchezo dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana na Al Hilal ya Sudan iliyopigwa mjini Khartoum, na baadae Arta Soler ya Djibout jijini Dar es salaam.
Kocha Zoran Maki amekiri kuvutiwa na uchezaji wa Kapama na ameahidi kumtumia katika kikosi chake cha kwanza miongoni mwa michezo ya Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa (Ligi ya Mabingwa Barani Afrika).
Amesema Michezo yote mitatu ya Kimataifa ya Kirafiki Kapama ameonyesha uwezo mkubwa na amejiridhisha ni mchezaji muhimu na ameanza kuwaamini katika kikosi chake.
“Mechi tatu amecheza vizuri sana tena ameonyesha ni mchezaji ambaye hategemei kucheza nafasi moja uwanjani, kwangu imenipa furaha kuona utayari wake huo, maana sio kila mtu yupo tayari kuchezeshwa maeneo tofauti na aliyozoea.”
“Baada ya kukosekana mechi mbili zilizopita naamini sasa ni muda kwake wa kupata nafasi, sikuweza kumtumia kwa haraka kwa sababu nilihitaji aingie kwenye kikosi huku akizoea taratibu kama ambavyo hata wachezaji wenzake wengi walianzia,” amesema Zoran Maki.
Nassoro Kapama alisajiliwa Simba SC mwishoni mwa msimu uliopita (2021/22) akitokea Kagera Sugar inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.