Mahakama ya Juu imetupilia mbali ombi la kutaka kuzuia kuapishwa kwa rais mteule William Ruto, lililowasilishwa na wanaharakati 11 wakipinga uapisho wa Ruto na naibu wake, Rigathi Gachagua kushika wadhifa huo kwa madai ya kukosa uadilifu.

Mahakama hiyo ya upeo, ilisema haina mamlaka ya kushughulikia mambo yaliyoibuliwa na wanaharakati hao, na kwamba iliwafaa kuwasilisha kesi hiyo katika Mahakama Kuu.

Majaji wa Mahakama ya Juu, kutoka kushoto ni Isaac Lenaola, Dkt. Smokin Wanjala, Philomena Mwilu, Martha Koome, Mohamed Ibrahim, Njoki Ndung’u na William Ouko. Picha na NMG.

Jana, Septemba 5, 2022 Mahakama hiyo ya juu nchini Kenya, iliidhinisha Uchaguzi wa William Ruto kuwa rais mteule baada ya kesi iliyowasilishwa na mpinzani wake katika uchaguzi mkuu, Raila Odinga kukosa ushahidi wa kutosha.

William Ruto, anatarajiwa kuapishwa Septemba 13, 2022, huku Rais Uhuru Kenyatta kupitia hotuba yake akisitiza kusimamia makabidhiano ya amani kwa utawala ujao, na katika hotuba akisema atazingatia sheria na kuheshimu maamuzi ya Mahakama.

Ajali ya basi: 45 wanusurika kifo
Madereva wapata elimu zoezi la ukaguzi magari ya Shule