Bei mpya za ukomo wa mafuta zilizotangazwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), Septemba 7, 2022 zitaanza kutumika hapo kesho Jumatano Sept 7, 2022.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Mkurungenzi Mkuu wa Ewura, Mhandisi Modestus Lumato imesema bei za mafuta zimeonekana kupungua baada ya kupanda mfululizo kwa miezi mitano kuanzia mwezi Aprili, 2022.
Mafuta ya Petroli, yatauzwa kwa Shilingi 2,969, Dizeli Shilingi 3,125 na mafuta ya taa yatauzwa kwa shilingi 3,535 kwa mkoa wa Dar es Salaam, tofauti na bei ya awali ya Shilingi 3, 410 kwa Petroli, dizeli Shilingi 3,322 na mafuta ya taa Shilingi 3,765 kwa lita.
Kushuka kwa bei za bidhaa hizo, kunatokana na kupungua kwa bei za mafuta katika soko la Dunia kwa mwezi Julai ambapo mafuta yatakayoanza kutumika kesho yalinunuliwa kipindi hicho.
Amesema, “Bei za mafuta katika soko la ndani zimepungua vilevile kwa kati ya Shilingi 271 kwa lita ya Dizeli na Shilingi 362 kwa lita ya petroli na Shilingi 430 kwa lita ya mafuta ya taa ukilinganisha na bei zenye ruzuku za Agosti 2022.”
Aidha, Lumato amefafanua kuwa, kwa mafuta ya dizeli ukiiacha bei ya Tanga ambayo inashuka kwa Shilingi 13 kwa lita, bei za Septemba 2022 zimeongezeka kwa Shilingi 37 kwa lita na Shilingi 86 kwa lita kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Mtwara.