Imefahamika kuwa Nahodha na Mshambuliaji wa Simba SC John Raphael Bocco alidhamiria kuondoka klabuni hapo, baada ya kuona hakuwa na thamani chini ya Kocha aliyeondoka Zoran Maki.

Bocco hakuwa na nafasi kwenye kikosi cha Zoran Maki, na badala yake alionekana kuwa chaguo la nne baada ya Washambuliaji Habib Kyombo, Dejan Georgijevic na Moses Phiri.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema Uongozi wa juu ulipambana kumshawishi Bocco kuendelea kubaki klabuni hapo, kutokanana kuamini uwezo na umuhimu wake kikosini.

Ahmed amesema mchakato wa kuhakikisha Bocco anabaki klabuni hapo, ulichukua nafasi kubwa siku chache kabla ya Dirisha la Usajili halijafungwa mwishoni mwa mwezi uliopita, huku akishinikiza mkataba wake usitishwe.

“Ilikua kazi kubwa iliyofanywa na viongozi wa juu kuhakikisha Bocco anabaki, alidhamiria kuondoka kwa sababu aliona hana thamani tena chini ya Kocha Zoran, kutokana na kukosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza mara kwa mara.”

“Hivyo Bocco hataondoka na badala yake ataendelea kuwepo msimu huu, kwani kati ya wachezaji wetu waandamizi tuliokuwa nao katika mipango mizuri ni yeye.”

“Amebaki baada ya kuridhishwa na ushawishi wa viongozi na ameridhia hilo, kwa sababu hata yeye amekiri kuipenda na kuthamini Simba SC, tunaamini utayari wake utaibua hisia chanya kwa wachezaji wenzake ili kukamilisha malengo tuliojiwekea msimu huu yanatimia.” amesema Ahmed Ally

Wachezaji wengine ambao wanatajwa walikaribia kuondoka Simba SC kabla ya Dirisha la Usajili kufungwa mwishoni mwa msimu uliopita ni Victor Akpan, Nassoro Kapama, Joash Onyango na Moses Phiri ambao hawakupendezwa na mipago ya Kocha Zoran Maki.

Ahueni bei mpya za Mafuta nchini
Kocha Zoran Maki aacha ujumbe Simba SC