Akiwa katika maandalizi ya kuelekea Pambano lake la Septemba 24 dhidi ya Bondia kutoka nchini Misri Abdo Khaleed, Bondia Twaha Kiduku amepokea taarifa njema kutoka kwa Mbunge wa Morogoro Mjini Abdulaziz Abood.
Twaha Kiduku atazichapa katika Pambano hilo la Kimataifa la kuwania mkanda wa UBO mjini Mtwara, huku Mashabiki wa Masumbwi Tanzania wakiwa na matumaini ya kuona akifanya vizuri.
Mbunge Abood ametangaza hadharani kumsaidia Kiduku katika maandalizi yake ili kumtia hamasa ya kutimiza jukumu la kuitetea Tanzania kwenye Pambano hilo la Kimataifa.
Amesema anapenda kuona vijana wanamichezo wanafanikiwa kwa maslahi yao na maslahi ya Taifa, hivyo amejitoa kwa hali na mali kumsaidia Bondia huyo anayetoka katika Jimbo lake, ili kumuwezesha kuwa na uhakika wa kwenda kupambana na kuibuka kidedea dhidi ya Mpinzani wake kutoka Misri.
“Twaha Kiduku anautangaza mkoa wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla, mimi ninapenda michezo na huyu ni mmoja wa vijana ambao wanastahili kusaidiwa ili kwenda kufanya vizuri katika Pambano lake”
“Nitahakikisha Twaha Kiduku anapata mahitaji yote muhimu ili aende kuleta ushindi kwa ajili ya Taifa letu.” amesema Abdulaziz Abood
Katika hatua nyingine Kiduku amemshukuru Mbunge Abood kwa kumuonyesha upendo na kumjali katika kipindi hiki ambacho anahitaji ushirikiano kutoka kwa watanzania na wadhamini mbalimbali.
Amesema kwa msaada huo anaamini atafanikisha lengo lake la kujiandaa kikamilifu, huku akiwaahidi watanzania kwa kusema hatawaangusha kwa sababu atapanda ulingoni kuitetea Bendera yao Septemba 24 mjini Mtwara.